Kamati ya Sera ya Fedha (Monetary Policy Committee—MPC) ilikutana tarehe 30 Januari  2023, kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha, mwenendo wa uchumi na mwelekeo wa sera  ya fedha. Kamati ilibaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha kwa mwezi Novemba na  Desemba ulikuwa na mafaniko. Kiwango cha ukwasi kilikuwa cha kutosha kwenye uchumi,  huku mikopo kwa sekta binafsi ikiendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu cha takribani  asilimia 21. Kasi hii ya ukuaji wa mikopo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwenye  ukuaji wa uchumi katika robo ya nne ya mwaka 2022. Vilevile, vigezo vilivyowekwa kwa ajili  programu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) kwa mwezi Desemba 2022, vilifikiwa.  

Kuhusu mwenendo wa uchumi, Kamati ilibaini kuwa changamoto za kiuchumi duniani  ziliendelea kuathiri shughuli za uzalishaji na kuongeza mfumuko wa bei nchini, japo kwa kasi  ndogo. Hii ni kutokana na kupungua kwa makali ya mvurugiko wa mnyororo wa ugavi na bei  za bidhaa katika soko la dunia, vikiambatana na hatua zilizochukuliwa na nchi mbalimbali  kwa ajili ya kupunguza athari za janga la UVIKO- 19. Pamoja na hayo, Kamati ilibaini kuwa: 

  1. mwenendo wa uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar ulikuwa wa kuridhisha katika  kipindi cha robo tatu za kwanza za mwaka 2022. Uchumi wa Tanzania Bara ulikua  kwa wastani wa asilimia 5.2, ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi  kama hicho mwaka 2021. Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, ujenzi  na uzalishaji viwandani. Kwa upande wa Zanzibar uchumi ulikua kwa asilimia 5.3  ukilinganishwa na asilimia 5.8, ukichangiwa zaidi na shughuli za malazi na chakula,  ujenzi, viwanda na upangishaji majengo. Kutokana na mwenendo huu na viashiria  vya kiuchumi katika robo ya nne ya mwaka 2022, Kamati inatarajia kuwa malengo ya  ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2022 yatafikiwa. Katika mwaka 2023, uchumi  unatarajiwa kuimarika zaidi kuliko mwaka uliopita kutokana na ongezeko la uwekezaji  wa sekta binafsi, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, uwekezaji wa Serikali kwenye  sekta za uzalishaji na miradi ya kimkakati, kuimarika kwa shughuli za utalii, pamoja  na mazingira ya biashara na sera wezeshi za fedha na bajeti. Vilevile, kuimarika kwa  mnyororo wa ugavi duniani kutachangia ukuaji huu; 

1 

  1. mfumuko wa bei uliongezeka kuendana na mwenendo wa bei za bidhaa kutoka nje  ya nchi, japo kasi ya ongezeko imepungua. Mfumuko wa bei kwa Tanzania bara  uliongezeka kufikia asilimia 4.9 mwezi Novemba 2022, kabla ya kupungua hadi  asilimia 4.8 mwezi uliofuata. Aidha, mfumuko wa bei ulikuwa chini ya lengo la asilimia  5.4 kwa mwaka 2022/23 na ndani ya vigezo vya mtangamano wa kiuchumi kwa nchi  wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa  Afrika (SADC) vya ukomo wa asilimia 8 na wigo wa asilimia 3-7, mtawalia. Mfumuko  wa bei kwa Zanzibar ulikuwa asilimia 7.8 na asilimia 8.1 kwa mwezi Novemba na  Desemba 2022, ukilinganishwa na lengo la asilimia 5. Aidha, Kamati ilibaini kuwa  katika chumi zote mbili, mfumuko wa bei ulikuwa mdogo kuliko nchi nyingi  wanachama wa EAC na SADC kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika  kupunguza athari za ongezeko la bei za bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi pamoja  na hatua za wananchi kutumia zaidi bidhaa mbadala kutoka ndani ya nchi. Hata  hivyo, mfumuko wa bei unarajiwa kushuka kutokana na kuanza kuimarika mnyororo  wa ugavi na matarajio ya ongezeko la uzalishaji chakula; 

iii. ujazi wa fedha kwa tafasri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 11.6 mwezi Desemba  2022, sambamba na lengo la asilimia 10.3 kwa mwaka 2022/23 kutokana na  kuendelea kuimarika kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Aidha, ukuaji huu  uliendana pia na malengo ya mfumuko wa bei ya asilimia 5.4; 

  1. ukusanyaji wa mapato ya Serikali ulifanyika kuendana na malengo katika kipindi cha  nusu ya kwanza ya mwaka 2022/23. Ukusanyaji wa mapato ya ndani ulikuwa mzuri  kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo makusanyo yalikuwa asilimia 96.7 na  asilimia 97.1 ya malengo, mtawalia. Matokeo haya yamechangiwa na kuimarika kwa  mifumo ya usimamizi wa ukusanyaji mapato na utayari wa walipa kodi. Matumizi ya  Serikali yalifanyika kuendana na malengo, sambamba uwekezaji kwenye sekta za  uzalishaji na ujenzi wa miundombinu, pamoja na kukabiliana na madhara yatokanayo  na athari mbalimbali za misukosuko ya uchumi wa dunia; 
  2. sekta ya nje iliendelea kuwa thabiti, licha ya changamoto za kiuchumi duniani zilizopelekea kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na  uhamishaji mali nchi za nje. Akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya kutosha  kugharamia takriban miezi 4.7 ya uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi. Kiwango hiki ni  ndani ya lengo la nchi la miezi isiyopungua minne na kigezo cha mtangamano wa  kiuchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha kuwa na  akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza angalau miezi minne na nusu; 
  3. sekta ya benki ilikuwa thabiti, yenye kiwango cha kutosha cha mitaji, ukwasi na yenye  kutengeneza faida. Rasilimali na amana ziliendelea kuongezeka kutokana na  kuimarika kwa mazingira ya kibiashara, pamoja na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kutoa huduma za fedha, ikiwemo kupitia huduma za uwakala. Kiwango cha 

2 

mikopo chechefu kiliendelea kupungua na kufikia asilimia 5.8 ya mikopo yote mwezi  Desemba 2022, kutoka asilimia 8.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Aidha  Kamati ilibaini na kutambua mafanikio haya kuzingatia kiwango cha asilimia 13 cha  mikopo chechefu kilichowahi kufikiwa mwaka 2017. Maendeleo haya yanatarajiwa  kuongeza kasi ya ukuaji wa mikopo nafuu kwa sekta binafsi na hivyo kuchochea  ukuaji wa Pato la Taifa. 

Kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi pamoja na matarajio katika nusu ya pili ya mwaka  2022/23, Kamati iliridhia Benki Kuu ya Tanzania kuendelea na utekelezaji wa sera ya  fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi kwa mwezi Januari na  Februari, 2023. Uamuzi huu unalenga kukabliana na ongezeko la mfumuko wa bei, pamoja na kuchochea kuimarika kwa shughuli za uchumi nchini. Aidha, utekelezaji huu  unaendana pia na mikakati iliyowekwa na Benki Kuu ili kufikia malengo ya sera ya fedha  yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF chini ya mpango wa ECF. Vilevile, Kamati  inatarajia kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 5.4, huku  sera ya fedha ikiendelea kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi na shughuli za  kiuchumi kwa ujumla. 

Gavana  

Benki Kuu ya Tanzania