Mbunge wa  jimbo la Arusha mjini ,Mashaka Gambo akizungumza kwenye mkutano huo wa wajasiriamali  jijini Arusha .
Mbunge wa  jimbo la Arusha mjini ,Mashaka Gambo akitembelea  moja ya banda la mjasiriamali  katika mkutano huo unaofanyika jijini Arusha.
Wajasiriamali  mbalimbali kutoka ndani na  nje ya nchi wakiwa katika picha ya pamoja na wadau pamoja na mbunge wa jimbo la Arusha mjini,Mashaka Gambo
……………………………………..
Julieth Laizer ,Arusha
Arusha.Wajasiriamali wadogo kutoka nchi za Afrika wamepatiwa elimu ya namna bora  ya kufanya biashara kimataifa ili waweze kujikwamua kiuchumi na kukuza biashara zao na hivyo kuweza kupanua wigo wa  kufanya  biashara kimataifa. 
 Wajasiriamali hao kutoka nchi za Afrika  hii leo wamekutana jijini Arusha kwa lengo la kujadili  na kutatua changamoto zinazo wakabili katika soko huru la Afrika .
Akizungumza   jijini Arusha  katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na shirika la CUTS International  ,Mshauri wa sera na biashara kutoka baraza la biashara la Afrika Mashariki  (EABC) Adrian Njau amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wajasiriamali  hao kujua  namna bora za kuboresha biashara  zao na kuweza  kufanya biashara ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa, mafunzo hayo ya uhalisi wa bidhaa na umuhimu wa kusafirisha bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi za Afrika kwa kutumia soko huru la Afrika na mambo ya viwango ni muhimu kwa wafanyabiashara wanaotaka kupata faida ndani ya soko hilo .
Njau alisema  kuwa,uondoaji wa vikwazo kwa wafanyabiashara wadogo ikiwemo kikwazo cha  kodi itawasaidia wafanyabiashara  kufanya biashara zao kwa ubora na ufanisi ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Mrisho  Gambo alisema kuwa, Serikali inayo fursa ya kumwezesha mfanyabiashara mdogo na kufanikiwa kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara  ndani na nje ya nchi.
Gambo alisema kuwa,kupitia  fursa hiyo ni wajibu wa  kila mmoja kuhakikisha anaitumia ipasavyo  ili waweze kuboresha  biashara  yake na kuweza kujulikana kimataifa kwa kuongezea  bidhaa husika thamani.