Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akizungumza katika mkutano wa hadhara baina ya wananchi wa kijiji cha Kibengu wilayani Mufindi mkoa wa Iringa na Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kibengu katika halmashauri ya wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara na Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula (katikati) akiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uuvi (wa pili kulia) , Naibu Waziri wa Maji Meryprisca Mahundi (Kulia) na Mkuu wa mkoa wa Iringa Halima Dendegu (kushoto) wakati Kamati ya Mawaziri Nane inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975 ilipowasili ofisi ya Mkuu wa mkoa Iringa kwa ziara ya siku moja mkoani humo. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
……………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewahimiza wananchi wa Mufindi mkoani Iringa kuhakikisha wanafuga ng’ombe wa maziwa kwa ajili ya kujipatia kipato.
Ulega alisema hayo Oktoba 26, 2022 wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975 ilipofanya ziara katika kijiji cha Kibengu wilayani Mufindi mkoa wa Iringa.
Akitolea mfano wa uwepo kiwanda cha maziwa cha Asasi mkoani Iringa kuwa, ni moja ya fursa kwa wananchi wa wilaya hiyo kuanza mchakato wa kuwa na ng’ombe wa maziwa kwa sababu upo uhitaji mkubwa wa maziwa hasa kipindi hiki ambacho kiwanda cha Asasi kinaongezwa na sambamba na kuwa na mpango wa kutengeneza maziwa ya unga.
“Iringa ni wakulima wazuri wa mahindi na miti, nashauri kila nyumba katika maeneo yake kuwa na ng’ombe wawili au watatu wa maziwa”. Alisema Ulega.
Aliongeza kwa kusema kuwa, ni vyema wananchi wa Mufindi na wilaya nyingine za mkoa huo wanapomaliza kutumia mahindi basi wawe na maziwa ambayo sehemu yanaweza kutumiwa na watoto na kiasi kingine kikatumika kwa ajili ya biashara. Alisema, katika jitihada ambayo wizara ya Mifugo na Uvuvi inaenda kufanya ni kuimarisha shamba lake la Sao Hill la Mitamba lilipo Iringa kwa lengo la kuboresha sekta ya mifugo.
Alisema, mbali na juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kuboresha sekta ya mifugo lakini moja ya jambo wizara yake itafanya ni kuzungumza na uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na kiwanda cha maziwa cha Asasi na Benki ya Kilimo pamoja na Shirika la PASS ni kuanzisha mradi ambao wale wananchi walio tayari basi waweze kukopeshwa ng’ombe wa maziwa ili wakati analima mahindi basi wawe pia na ng’ombe wa maziwa na baadaye kuwa na vituo vya kukusanya maziwa, jambo litakalowapa uhakika wa kila siku kupata takriban shilingi 10,000.