MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk.Alphonce Chandika,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Hospitali hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 25,2022 jijini Dodoma.
…………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk.Alphonce Chandika,amesema kuwa wameokoa zaidi ya Shilingi bilioni nne za matibabu ya wagonjwa wa figo,nyonga na magoti ambao wangetibiwa nje ya nchini.
Hayo ameyasema leo Oktoba 26,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Hospitali hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Dk. Chandika, amesema kwenye upandikizaji wa figo, wananchi 31 wamenufaika na huduma hiyo na kuokoa Sh.Bilioni 2.3.
”Tumefanikiwa kuanzisha huduma za upandikizaji wa figo na jumla ya wananchi 31 wamenufaika na huduma hiyo, huku gharama ya huduma hiyo ikiwa ni takriban shilingi milioni 25 wakati India angetibiwa kwa takriban Shilingi milioni 100 ambapo kwa wagonjwa hao 31, Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi bilioni 2.3”amesema Dk.Chandika
Amesema kuwa Hospitali hiyo imefanikiwa kutoa huduma za matibabu ya moyo ambapo kuna maabara maalum inayotumika katika kutoa matibabu ya moyo pasipo kufungua kifua.
“Hospitali hii ni ya pili hapa nchini kutoa huduma hii.Tangu huduma hii imeanza kutolewa mwaka 2019, jumla ya wananchi 715 wamehudumiwa kwa kuchunguzwa,”Amesema Dkt.Chandika
Amesema kuwa wagonjwa 39 waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo wamehudumiwa kwa kuwekewa vipandikizi na kati ya 39, wagonjwa wawili kati yao walihudumiwa kwa dharura ambapo kama ingekuwa ni kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu Dar es Salaam wangepoteza maisha.
“Kuna wagonjwa nane ambao mapigo yao ya moyo yanashuka sana, walihudumiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kupandikizwa betri kwenye moyo na kupitia maabara hiyo tumeweza kuhudumia watoto 14 waliozaliwa na matatizo ya moyo,”Amesema Dkt.Chandika
Na kuongeza kuwa “Hospitali imeanza kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliobainika kuwa na matatizo ya kuzaliwa ya moyo ambapo tayari watoto kumi wameshahudumiwa,”Amesema Dkt.Chandika
Pia tangu mwaka 2020, Hospitali ilifanikiwa kuanzisha upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka vipandikizi, hadi sasa jumla ya wagonjwa 56 wamewekewa vipandikizi hivyo kwa wastani wa gharama ya shilingi milioni 12. Gharama za huduma hii nchi za nje ni takriban milioni 35 ambapo kwa wagonjwa 56 waliohudumiwa , Serikali imeokoa jumla ya Shilingi bilioni 1.28
“Hospitali hii ndio pekee nchini imefanikiwa kuanzisha huduma ya uvunjaji wa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi na miale pasipo kumfanyia mgonjwa upasuaji, huduma hii imeshatolewa kwa wagonjwa 148 kwa gharama ya Shilingi milioni 1.2 kwa mgonjwa mmoja, kwa nje ya nchi gharama ni zaidi ya milioni 7 ambapo kwa wagonjwa 148, Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 850,”Ameeleza Dkt.Chandika
Katika jitihada za Serikali kuhakikisha inawaletea wananchi huduma za afya zilizo bora, ilidhamiria kuiwezesha Hospitali ya Benjamini Mkapa kuwa na vifaa tiba vya kisasa na vinavyotumia teknolojia ya kisasa ili iweze kukidhi adhma yake ya kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia matibabu ya kiwango cha juu.
Dkt.Chandika amesema kwa mwaka 2022/23 hospitali hiyo imeanza ujenzi wa kituo cha mionzi cha matibabu ya saratani ambapo wamepokea Sh.Bilioni 10.
“Pia huduma ya upandikizaji wa uboho tuliomba kuwezeshwa Sh.Bilioni moja tumepewa na matibabu yataanza Januari 2023,”amesema