Mkuu wa mkoa wa  Arusha,John Mongella  akizungumza katika hafla hiyo  jijini Arusha leo,pembeni yake ni  Meneja wa TARURA mkoa wa Arusha,Mhandisi Laynas Sanya
Meneja wa TARURA  mkoa wa  Arusha, Mhandisi  Laynas Sanya akizungumza  na waandishi wa  habari jijini Arusha 
Baadhi ya washiriki wakiwa katika picha ya pamoja kwenye kikao hicho jijini Arusha leo. 
***********************
 
Julieth Laizer,Arusha.
 
Arusha.Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amewataka wakandarasi 18 waliosaini mikataba  ya kutengeneza miundo mbinu ya barabara na madaraja mkoani hapa, kufanya kazi kwa weledi na  uzalendo kwa kuzingatia muda na wale watakaoenda kinyume ametishia kuwafutia kufanyakazi katika mkoa huo.
 
Mongela ameyasema hayo  leo wakati alipokuwa akishuhudia utiaji saini wa mikataba 18 yenye thamani ya sh,bilioni 4 kati ya Wakala wa barabara vijijini na Mijini ( TARURA) na wakandarasi 18 ,ikiwa ni fedha za nyongeza zilizotokana na tozo.
 
Katika hatua hiyo Mongella amewataka wakandarasi hao kufanyakazi kwa  kufuata miongozo iliyopo kwenye mikataba yao , kwa kutekeleza mradi kwa viwango na kuepuka ubabaishaji, ucheleweshaji na kutokidhi ubora wa mradi.
 
Amesema, kukamilisha kwa barabara hizo kwa wakati na kwa viwango kutasaidia kushusha gharama za maisha kwa wananchi.
 
Aidha, amewaelekeza TARURA wakawasimamie wakandarasi hao kwa ukaribu zaidi ili wakamilishe miradi hiyo kwa wakati.
 
Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha mhandisi  Laynas Sanya amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 walipatiwa jumla ya fedha za matengenezo ya barabara  zaidi ya  bilioni 18 kwa awamu ya pili na katika awamu ya kwanza mikataba 34 ilisainiwa yenye  thamani ya bilioni 14.
 
Amesema  awamu ya pili ya utiaji saini  jumla ya mikataba 18 yenye thamani ya zaidi ya sh,bilioni 4.071,921,007.26 imesainiwa na wakandarasi mbalimbali wazawa watakaotekelez miradi ya miezi sita kwa kiwando na ubora wa hali ya juu.
 
“Mikataba hii tumesaini ikiwa ni kufuata mwongozo wa rais Samia suluhu ambaye alielekeza mikataba yote isainiwe hadharani bila kusiri wowote”.
 
Amesema wakati wa utekelezaji wa miradi ya barabara mwongozo wa serikali unawaka pia waweke taa za  barabarani jambo ambalo alisisitiza  wameanza kulitekeleza.
 
“Mikataba iliyosainiwa leo ni kutengeneza barabara kwa kiwango cha Lami,ujenzi wa makaravati,ujenzi wa madaraja ya mawe ,uj3nzi wa mifereji na matengenezo ya kawaida ya barabara”.
 
Hata hivyo amesisitiza kuwa Tarura itahakikisha inawasimamia wakandarasi hao kuhakikisha miradi hiyo inatengenezwa kwa kiwango cha juu na kukamilika kwa wakati ndani ya miezi sita.
 
Naye, Mmoja ya wakandarasi Rashidi Sevingi  kutoka kampuni ya Raly (EA) Limited ameishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapatia kandarasi hizo kwani hapo awali walizoea kuona kandarasi nyingi zinakwenda kwa makapuni ya kigeni.
 
Amewasihi wakandarasi wenzake  kutekeleza mikataba waliyosaini kwa weledi ili waendelee kuaminiwa zaidi na Serikali .