Tanzania
ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya maji na
usafi wa mazingira nchini ili kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini
kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama. 

 

Hayo
yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Dkt. Stergomena Tax leo tarehe 17 Oktoba 2022 alipotembelea Chuo Kikuu cha
Sayansi za Maisha cha Warsaw nchini Poland katika siku yake ya kwanza ya ziara
ya kikazi nchini humo.

 

Mhe.
Dkt. Tax ambaye alikutana na Menejimenti ya Chuo hicho pamoja na wamiliki wa
kampuni mbalimbali za Poland zenye nia ya kuwekeza katika sekta ya maji nchini,
amesema, sekta ya maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele
nchini, kwani zinagusa maisha ya wananchi wote wa mijini na vijijini na
kwamba  wanahitajika wawekezaji makini na
wenye tija kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendelea kuiboresha.

 

Amesema
miji mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma na Dar es Salaam inaendelea kukua kwa
kasi hivyo upo umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo ili kuwawezesha
wananchi kupata maji safi na salama lakini pia kuendelea kutunza mazingira.

 

“Maji
na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa   Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi
wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tutaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali ili kuhakikisha sekta hii
inaboreshwa zaidi hususan kwenye teknolojia ya kisasa ya usimamizi wa maji  ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalam
wetu” alisema Dkt. Tax.

 

Pia
amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea
kushirikiana na  Taasisi mbalimbali
zinazosimamia sekta ya maji nchini ikiwemo Wizara ya Maji ili kwa pamoja
kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili
sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi.

 

Awali
akimkaribisha Mhe. Waziri chuoni hapo, Mkuu wa Chuo, Prof. Michal Zasada
amesema chuo hicho ambacho kimejikita katika ufundishaji wa Teknolojia mpya ya
usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, kipo tayari kushirikiana na
Tanzania katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wa sekta hiyo kutoka
nchini.

 

“Tumefarijika
kutembelewa na wewe Mhe. Waziri na ujumbe wako kutoka Tanzania. Chuo chetu
kinatoa kozi mbalimbali za Shahada na Shahada ya Uzamili katika masuala
mbalimbali ikiwemo sekta ya maji. Tayari wataalam kadhaa kutoka sekta ya maji
wamewahi kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo hapa chuoni. Tunaendelea
kuwakaribisha Watanzania kujiunga na program mbalimbali za mafunzo hususan za
sekta ya maji zinazotolewa chuoni hapa” alisema Prof.  Zasada.

 

Wakati
wa Mkutano huo Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na sekta ya maji na usafi
wa mazingira za Poland ikiwemo ile ya Asseco ziliwasilisha mada na kueleza
utayari wao wa kuwekeza katika sekta ya maji kwa kuanza na miji ya Dodoma na
Dar es Salaam.

 

Akiwa
chuoni hapo Mhe. Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea maabara za kisasa za
usimamizi wa maji pamoja na  kujionea mradi
wa maji unaotumia teknolojia ya kisasa unaotekelezwa na chuo hicho.

 

Mhe.
Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi
19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano
wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Maisha cha Warsaw nchini Poland, Prof. Michal Zasada mara baada ya kuwasili Chuoni hapo leo tarehe 17 Oktoba 2022. Pamoja na ambo mengine Mhe. Waziri Tax alizungumza na menejimenti ya chuo hicho kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya elimu na maji pamoja na kutembelea miradi ya maji inayotekeelzwa na chuo hicho. Mhe. Dkt. Tax yupo nchini poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2022   

Mhe Waziri Dkt. Tax akizungumza na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw cha nchini Poland kuhusu masuala ya ushirikiano katika sekta za elimu na maji. Kushoto kwake ni Prof. Zasada, Mkuu wa Chuo hicho akifuatiwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Marta Mendel na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Mhe. Krystof Buzalski. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani anayewakilisha pia nchini Poland, Mhe. Balozi Abdallah Possi

Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Zasada akizungumza kumkaribisha Mhe. Dkt Tax alipotembelea Chuoni hapo 
 
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia) akiwa pamoja na Wajumbe kutoka Tanzania walioambata na Mhe. Waziri Tax nchini Poland.
 
Sehemu ya Wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw na wamiliki wa Kampuni zinazojishughulisha na masuala ya maji wakifuatilia kikao
 
Sehemu nyingine ya Wajumbe kutoka Tanzania 

 

Sehemu ya washirki kutoka Chuoni hapo

 

Sehemu ya Washiriki kutoka Tanzania

 

Mkutano ukiendelea

 

Sehemu ya wajumbe kutoka Chuoni hapo
 
Sehemu nyingine ya washiriki

 

Mada kuhusu masuala ya maji na usafi wa mazingir aikiwasilishwa na mmoja wa washiriki kutoka Poland
 
Mhe. Dkt. Tax akimweleza Prof. Zasada kuhusu zawadi  kutoka Tanzania kabla ya kumkabidhi. Zawadi hiyo ni mkusanyiko wa bidhaa za Tanzania zikiwemo Kahawa, Korosho, batiki, Vikoi na Viungo vya chakula.
 

 

Prof. Zasada naye akimkabidhi zawadi Mhe. Waziri Dkt. Tax
Picha ya pamoja
Mhe. Dkt. Tax akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kituo cha Maji kilicho chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, Prof. Wojciech Sas alipofika kukitembelea kituo hicho na kujionea maabara mbalimbali za maji

 

Mhe. Dkt Tax na ujumbe wake wakipata maelezo kutoka kwa mtaalam wa mitambo na teknolojia mbalimbali za maji Prof. Adam Kiszko
 

 

Mhe. Dkt. Tax akipata maelezo kutoka kwa mtaalam wa maabara ya maji alipotembelea maabara hiyo

 

Mhe. Dkt. Tax akiangalia bwawa lililochimbwa kitaalam bila kuharibu mazingira na viumbehai  alipotembelea Kituo cha Maji kilicho chini ya Chuo Kikuu cha Sayansi za maisha cha Warsaw, Poland