……………………..
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
WAZAZI Mkoani Pwani wameaswa kuwa karibu na watoto pamoja na kuwaonya tabia ambazo zinaashiria maadili yasiyo mema kwenye jamii ili kujiepusha na tabia ya udokozi,makundi ya kiuhalifu kama panyaroad na kukaa mitaani kuvuta bangi.
Akizungumza na wanafunzi,walimu na wazazi wakati wa sherehe ya kuwaaga wahitimu wa darasa la Saba shule ya Msingi Kips na Kips Anex, zilizopo Kibaha ,sheikh mkuu wa mkoa alhaj Hamis Mtupa alieleza, mtoto alelewavyo ndivyo akuavyo,hivyo wazazi na walezi wakiwa waoga kusema na watoto wao itazalisha kundi kubwa la watoto wenye maadili mabovu.
Mtupa alieleza, wazazi wanapaswa kuwekeza kwenye elimu kwa watoto ili kuwa na kipindi kirefu Cha kujisomea ama kujifunza mambo yenye manufaa kwao.
“Wazazi wawekeze kwenye elimu ya watoto badala ya kutumia fedha zao katika anasa na shughuli zisizo na faida lakini wakiwekeza kwenye elimu ya watoto ambao watakuja kuwasaidia wao baadaye “alisema Mtupa.
Alisema baadhi ya watoto wamekuwa wakijiunga na makundi ya kihalifu kutokana na kutosimamiwa tangu awali.
“Unakuta mzazi anaogopa mtoto badala ya mtoto kuogopa mzazi, watoto wa siku hizi hawasemwi ,kila kitu wanajua wao, wengine hawapelekwi shule hali inayopelekea kujiingiza kwenye mambo mabaya na ya uhalifu.
Nae Meneja wa shule hiyo Nuru Mfinanga alisema kuwa wazazi wasiwaingize kwenye migogoro ya kifamilia watoto wao kwani husababisha kuathirika kisaikolojia.
Nuru alieleza, watoto wanapoingizwa kwenye migogoro ya kifamilia hawawezi kufanya vizuri kwenye masomo yao .
“Wazazi migogoro yenu malizeni faragha,msihusishe watoto,wanajikuta wanashindwa kusoma vizuri darasani, mtoto unakuta anawaza magomvi ya wazazi badala ya kusoma”alisisitiza Nuru.
Mkurugenzi wa shule hizo Alhaj Yusuph Mfinanga aliwaomba wazazi kulipa ada kwa wakati ili ziweze kuendesha shughuli za shule.
Mfinanga alisema kuwa fedha hizo pia zinasaidia kutoa motisha kwa walimu hivyo ili matokeo yaendelee kuwa mazuri lazima wazazi walipe ada kwa wakati.
Kwa upande wa wanafunzi wa shule hiyo Herieth Kapinga alieleza,wamefanya vizuri mitihani yao ya kumaliza elimu ya Msingi wanaamini ufaulu wao utakuwa mzuri kutokana na kuandaliwa mazingira mazuri ya usomaji.
Picha mbalimbali za tukio la sherehe za darasa la Saba katika shule ya msingi Kips.