Waziri wa maliasili na utalii  Balozi Dk Pindi  Chana  akizungumza  na waandishi  wa habari jijini Arusha juu ya maandalizi ya mkutano  jijini Arusha
************************
Julieth Laizer, Arusha.
Arusha.RAIS wa jamhuri  ya muungano  wa  Tanzania ,Samia  Suluhu Hassan anatarajiwa  kufungua  mkutano wa 65 wa shirika la utalii duniani -Kamisheni ya Afrika (UNWTO -CAF) ambalo Tanzania ni mwanachama wake tangu mwaka 1975 utakaofanyika  oktoba 5 hadi 7 jijini Arusha. 
Hayo yamesemwa  leo   jijini Arusha na Waziri wa maliasili na utalii ,Balozi Dk  Pindi  Chana wakati akizungumza  na waandishi wa  habari jijini Arusha. 
Balozi Chana amesema kuwa,mkutano huo  unatarajiwa kukutanisha mawaziri wenye shamans ya maswala ya utalii na maliasili kutoka nchi wanachama wa UNWTO  wa kanda ya Afrika zaidi ya 50 kujadili kuhusu mustakabali wa ustawi wa maendeleo  ya sekta ya utalii barani Afrika hasa baada ya athari za mlipuko wa janga la UVIKO -19 iliyokuwa imeathiri utalii wa Tanzania. 
Amesema kuwa,mkutano huo utahusisha wadau wengine wakiwemo  watalaamu wa utalii na ukarimu katika ngazi  ya kimataifa  na kikanda, watoa  huduma mbalimbali katika mnyororo  wa utalii,wawekezaji, pamoja na watu mashuhuri  zaidi ya 150.
“Kauli mbiu  ya mkutano huu ni Rebuilding Africa’s Tourism Resilience for Inclusive Socio-Economic Development “na utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa shirika hilo Zurab Pololikashvili  “amesema Dk Chana. 
Ameongeza kuwa,Tanzania ilichanguliwa kuwa mwenyewe wa  mkutano  wa 65 wa  UNWTO kupitia mkutano wa 64 uliofanyika septemba 2021 nchini Cabo Verde .
Amefafanua kuwa, katika mkutano huo  patafanyika  matukio mbalimbali ambayo ni  pamoja na jukwaa la uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji  zilizopo  nchini na uzinduzi wa  Investment  Guideline(Tourism doing Business)Marketing Symposium kwa ajili ya kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu maswala ya masoko .
Amesema kuwa,kulingana na sera ya  Taifa ya utalii (1999) mkutano huo ni muhimu kwa  kuwa ni mojawapo ya jitihada za serikali katika kuongeza idadi  ya watalii na kupanua  wigo  wa mazao ya utalii nchini kupitia  uendelezaji wa  mazao ya utalii  ya kimkakati  hususani  wa  mikutano na matukio  .
Balozi Dk Chana amesema kuwa ,mkutano  huo  utawezesha kujengea uwezo  watalaamu  na wadau wa utalii katika kutangaza utalii,kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii katika kanda mbalimbali za utalii nchini kulingana na shabana ya kuongeza idadi ya watalii kufikia watalii milioni 5 na mapato ya Dola  za Marekani  Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa  Arusha ,John Mongela  amesema kuwa,mkoa umejipanga kikamilifu kuhakikisha mkutano huo unaofanyika salama na wananchi wa  Arusha wananufaika kupitia mkutano huo  .
Aidha Mongela amesema kuwa mkutano huo utatoka fursa sio kwa wanaarusha tu bali dunia na Afrika kwa ujumla  kwani juhudi  zilizofanywa na Rais za kutangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour ni kubwa sana na linapaswa kuungwa mkono.