Home Uncategorized MKURUGENZI BENKI YA DUNIA ARIDHISHWA NA KASI YA UBORESHAJI HUDUMA ZA MAHAKAMA

MKURUGENZI BENKI YA DUNIA ARIDHISHWA NA KASI YA UBORESHAJI HUDUMA ZA MAHAKAMA

0
Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika anayeshughulikia Ukuzaji wa Uchumi na Taasisi kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Asad Alam akisaini kitabu cha wageni alipofika ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 28 Septemba, 2022 kwa ajili ya ziara fupi ya kufahamu maendeleo ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika anayeshughulikia Ukuzaji wa Uchumi na Taasisi kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Asad Alam alipowasili katika Ofisi ya Mtendaji huyo  iliyopo Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi huyo amefanya ziara fupi ya kutembelea Mahakama leo tarehe 28 Septemba, 2022.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika anayeshughulikia Ukuzaji wa Uchumi na Taasisi kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Asad Alam (wa tano kulia) pamoja na sehemu ya Maafisa wa Mahakama na Maafisa kutoka Benki ya Dunia walioambatana na Mkurugenzi huyo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwaonesha Maafisa kutoka Benki ya dunia namna ya shauri linavyoendeshwa kwa njia ya mkutano mtandao ‘video conference’ jana tarehe 28 Septemba, 2022 katika Kituo cha Taarifa kilichopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu-Dar es Salaam.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (aliyenyoosha mkono) akimuonesha Bw. Alam (aliyesimama wa kwanza kulia kwa Msajili) gari maalum la Mahakama inayotembea alipotembelea Mahakama Kuu-Kituo Maalum cha Masuala ya Familia kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa tano kushoto), Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika anayeshughulikia Ukuzaji wa Uchumi na Taasisi kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Asad Alam pamoja na sehemu ya Maafisa wa Mahakama na wa Benki ya Dunia (WB) wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya Mahakama inayotembea wakati Mkurugenzi huyo alipoitembelea jana tarehe 28 Septemba, 2022 akiwa katika ziara yake.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama ya Tanzania, Bw. Daniel Msangi (aliyesimama) akiwasilisha Mada ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB). Wasilisho hilo limetolewa kwa ugeni kutoka Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika anayeshughulikia Ukuzaji wa Uchumi na Taasisi kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Asad Alam (hayupo katika picha).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta (katikati), Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika anayeshughulikia Ukuzaji wa Uchumi na Taasisi kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Asad Alam (kulia) wakifurahia jambo.

 Meneja kutoka Benki ya Dunia (WB) anayeshughulikia masuala ya Utawala na menejimenti ya Fedha, Bw. Manuel Vargas akichangia jambo wakati wa wasilisho la Mada ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Bw. Daniel Msangi (hayupo katika picha).


Picha ya pamoja mbele ya Kituo Jumuisha cha Masuala ya familia Temeke.

(Picha na Castilia Mwanossa, SAUT)
………………………………..
 
Na Mary Gwera, Mahakama

Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika anayeshughulikia Ukuzaji wa Uchumi na Taasisi kutoka Benki ya Dunia (WB), Bw. Asad Alam amepongeza hatua ya uboreshaji wa huduma za utoaji haki nchini huku akiahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuiwezesha Mahakama kuendelea kuhudumia wananchi.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara yake fupi aliyofanya Mahakama jana tarehe 28 Septemba, 2022, Bw. Alam alikiri kuridhishwa na hatua ambayo Mahakama imepiga hususani katika uboreshaji wa Miundombinu ya majengo, uanzishwaji wa huduma za Mahakama inayotembea na matumizi ya Mkutano mtandao ‘Video Conference’ katika uendeshaji wa mashauri.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kutembelea Mahakama ya Tanzania, lengo la kuja kwangu ni kujionea jinsi mnavyotekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama, nina furaha kusema kuwa kwa taarifa iliyotolewa na kutembelea jengo la Mahakama hii ya Temeke na kujionea uendeshaji wa Mashauri kwa njia ya mkutano mtandao ninaweza kusema kuwa mmepiga hatua na mnafanya vizuri, hivyo, Benki ya Dunia itaendelea kuwezesha uboreshaji zaidi wa huduma,” amesema.

Mbali na pongezi, Mkurugenzi huyo alisema kuwa, kuna haja ya kusogeza zaidi huduma za utoaji kwa wananchi waliopo katika maeneo ya mbali zaidi huku akisisitiza kuhusu kutosahau kuzingatia usawa wa jinsia huku akisisitiza kuwa ni muhimu pia kuwafikia wanawake.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amemuhakikishia Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia kuwa, huduma zinazotolewa na Mahakama zinamlenga mwananchi na katika awamu ya pili ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki hiyo, Mahakama imepanga kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa (9) ili huduma ya Mahakama iweze kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

“Napenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais wa awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiamini Mahakama na kuiwezesha kupata mkopo kutoka Benki ya Dunia, na katika awamu hii ya pili tunatarajia kujenga Vituo vya Utoaji Haki tisa (9) na tumepanga kujibana zaidi ikibidi tupate hata Vituo hivyo 12 ili tuweze kuwafikia wananchi wengi zaidi,” ameeleza Prof. Ole Gabriel.

Mtendaji Mkuu ameishukuru pia Benki ya Dunia kwa kuongeza kiwango cha fedha za Mradi ambazo ni Dola za Kimarekani Milioni 90 sawa na Bilioni 210 za kitanzania  zitakazosaidia kuboresha zaidi huduma za kimahakama ikiwemo kuongeza idadi ya Mahakama zinazotembea ‘Mobile Courts’, majengo ya Mahakama, kuongeza matumizi ya mkutano mtandao ‘Video Conference’ katika uendeshaji wa Mashauri na kadhalika.

Akiwasilisha Mada kwa Mkurugenzi huyo na Maafisa alioambatana nao, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Bw. Daniel Msangi amesema kuwa, tangu kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama umesaidia kupatikana kwa mafanikio lukuki ikiwemo kusogeza huduma karibu na wananchi huku akitoa mfano kuwa, upatikanaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro umewapunguzia wananchi aza ya kusafiri umbali mrefu kuja Dar es Salaam kupata huduma ya ngazi hiyo ya Mahakama.

Akizungumzia Kituo maalum cha Masuala ya Familia Temeke, Bw. Msangi ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake Mahakama hiyo maalum iliyoanza kufanya kazi tarehe 25 Oktoba, 2022 imehudumia jumla ya wananchi 124,476 wanawake wakiwa 66,222 na wanaume 58,254.

Ameongeza kuwa, faida nyingine ni utoaji wa huduma kupitia Mahakama zinazotembea ambazo kwa sasa zipo mbili (2) zinazotoa huduma Dar es Salaam na Mwanza, amebainisha kuwa, kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu Mahakama hizo zimehudumia wananchi wapatao 12, 810, kati ya hao Wanawake ni 7,236 na Wanaume ni 5,574.

Waambata wa Mkuu huo, nao kwa pamoja wamepongeza Uongozi wa Mahakama kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa Huduma za Mahakama. Katika ziara yake fupi Mkurugenzi huyo alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,  kutembelea Kituo cha Taarifa cha Mahakama kilichopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu ambapo walishuhudia shauri likiendeshwa kwa Mkutano Mtandao ‘Video Conference’.

Alihitimisha ziara yake fupi kwa kutembelea na kukagua Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, kukagua na kupata taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court’ pamoja na taarifa ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.