Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Relief Initiatives, Edwin Mugambila na ACP
Ahmad Mwendadi kutoka sekretariat ya kitaifa ya kupambana na Biashara ya
Usafirishaji Haramu wa Binadamu nchini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stellah Mutabihirwa, Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Allu Nzowa na SSI Felista Orden
Sanga- Superintendent wa Uhamiaji Mkoa wa Singida,
Dotto Mwaibale na Philemon Mazalla, Singida
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi
wa Polisi (ACP) Stellah Mutahibirwa amesema mapambano ya kutokomeza biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu yatafanikiwa kwa ushirikiano baina ya Uhamiaji,
Ustawi wa Jamii na jeshi la polisi idara ya dawati la jinsia.
Mutahibirwa ameyasema hayo leo wakati akifungua
semina ya siku nne iliyoanza leo Septemba 13 hadi Septemba 16 iliyowahusisha
wasimamizi wa sheria mahakama, polisi, uhamiaji na ustawi wa jamii kwa lengo la
kuwajengea uwezo wa uelewa wa namna ya kushughulikia utokomezaji wa biashara
hiyo semina ambayo imeandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania
Relief Initiatives.
“Ushirikiano wa makundi haya ni muhimu sana
ili kutokomeza biashara hii ambayo inakuwa kwa kasi na kuwahusisha watoto wenye
umri kati ya miaka 12 hadi 15 na Mkoa wa Singida ukiwa ni miongoni mwa mikoa
iliyoathiriwa na biashara hii” alisema Mutahibirwa
Mutahibirwa aliomba idara ya uhamiaji
kujiridhisha ipasavyo utoaji wa hati za kusafiria zinazoombwa kwa ajili ya
watoto wa lika hilo kwenda nje ya nchi na wanakwenda kufanya nini.
“Watoto
wengi wamekuwa wakichukuliwa majumbani na kupelekwa kusikojulikana kwa kigezo
cha kwenda kutafutiwa ajira, lakini ukijaribu kufuatilia utakuta wengi huishia
kupelekwa kwenye majumba ya starehe, na wengine kufanyishwa biashara za ukahaba
kwenye maeneo mbalimbali kama kivutio cha biashara za watu kinyume na matarajio
na bila ridhaa yao,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Relief
Initiatives, Edwin Mugambila alisema hali ni mbaya na kuwa biashara hiyo hivi
sasa ipo mikoa yote lakini iliyoathiriwa zaidi ni ile ya pembezoni kutokana na
muingiliano wa watu na ndiyo maana wamekuwa wakifanya semina hizo katika mikoa
yote ili kuwajengea uelewa wananchi.
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Singida Phaustine Ngunge
alisema ili kukabiliana na tatizo la biashara hiyo haramu, pamoja na
mambo mengine inahitajika zaidi kutolewa kwa elimu kwa wananchi na sheria
ziangaliwe upya.