Wizara ya Kilimo inapenda kuutaarifu Umma na Wafanyabiashara wote wa Mazao ya Chakula kuwa, haijasitisha utoaji wa vibali vya kusafirisha Mazao ya Chakula kwenda nje ya nchi kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Wizara ya kilimo kwa kufuata taratibu zote za kisheria imeendelea kutoa vibali vya kusafirisha Mazao ya Chakula kwenda nje ya nchi kupitia mfumo wa utoaji vibali wa kielektroniki.
Katika kipindi cha kuanzia tarehe 27 Agosti hadi 7 Septemba, 2022, Wizara imetoa vibali vya Mahindi, Maharage,Unga, na Mchele kwenda nje ya nchi vyenye jumla ya Tani 37,450.
Hata hivyo, Wizara ya Kilimo inapenda kuwasisitiza wafanyabiashara wa mazao ya chakula kwenda nje ya nchi(Export) au kuingiza ndani ya nchi(Import) kufuata taratibu zifuatazo:
- Kampuni inapaswa kuwa;
- Imesajiliwa na BRELA au kwa kuzingatia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
- Leseni halali ya kufanya biashara ya Mazao ya Chakula
- Nyaraka za kulipa kodi(Tax Clearance Certificate)
- Risiti ya EFD ya malipo kutoka Halmashauri husika
- Kuwasilisha Release Order Certificate wakati wa kuomba kibali(Export permit) cha kusafirisha Mazao.
- Aidha, Wizara inawakumbusha wafanyabiashara wa Mazao ya Chakula kuwa, ili kuepuka usumbufu usio wa lazima, wanatakiwa kuwa na kibali cha kusafirisha Mazao nje ya nchi(Export Permit) au kuingiza ndani ya nchi(Import Permit) kabla ya kufikisha mzigo Mpakani, Bandarini, au Kiwanja cha ndege.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Kilimo.