MENEJA wa Menejimenti ya Maarifa na Mawasiliano kutoka taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt.Richard Kasuga,akizungumz na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 11,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu shughuli za taasisi hiyo na Vipaumbele vyake kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
……………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa mbegu kutoka tani milioni 226 hadi tani milioni 1453.
Hayo yamesemwa leo Agosti 11,2022 jijini Dodoma na Meneja wa Menejimenti ya Maarifa na Mawasiliano kutoka taasisi hiyo Dkt.Richard Kasuga,akizungumz na waandishi wa habari leo Agosti 11,2022 jijini Dodoma kuhusu shughuli za taasisi hiyo na Vipaumbele kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
Dk.Kasuga amesema ni kutokana na bajeti ya Serikali kuongezwa kutoka Bili 11.63 hadi bilioni 40 mpka bilioni 54 ambapo mpango ni kuzalisha tani za mbengu mil 226 hadi tani mil1453.
Aidha,amesema kuna mpango wa upanuzi uzalishaji wa tani 17000 za Pamba huku uzalishaji wa mazao ya asili ikiwemo Mihogo na mazao mengine tani milioni 50.
”TARI imejipanga katika utekelezaji wa uzalishaji kufikia asilimia 34% ya wakulima waweze kupata teknolojia sahihi na kuongeza uzalishaji wa eneo ambapo mahindi ni kufikia tani 4 kutoka tani moja”amesema Dk.Kasuga
Aidha amesema kuwa katika kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kupikia nchini mikoa iliyopewa kipaumbele cha uzalishaji zao la alizeti ni pamoja na Singida,Dodoma na Simiyu.
Pia,ametoa wito kwa wakulima kulima hasa mkoa wa Dodoma kulima kwa kufuata taratibu za kitaalam ili kuzalisha Zabibu zenye ubora zaidi.
Ameongeza kuwa teknolojia zingine zitakazogunduliwa ni za uongezaji thamani katika mnyororo wa thamani wa mazao, kuboresha afya ya udongo, kugundua mbinu bora za ukuzaji mazao, zana bora za kilimo, na utunzaji wa mazao baada ya mavuno na kuimarisha uchumi jamii.
“Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 jumla ya teknolojia 35 zitazalishwa kati ya hizo 15 ni mbegu bora, tano agronomia, tano afya ya udongo na 10 teknolojia baada ya mavuno. wakulima 5,000 na Maafisa Ugani 500 watapatiwa mafunzo ya kilimo bora cha mazao mbalimbali na wasindikaji 2,000,000 watapatiwa teknolojia mpya za kuongeza thamani yak mazao,”ameeleza Dk.Richard Kasuga
KUIMARISHA MAABARA ZA UTAFITI
Dk.Kasuga amesema katika mwaka huu wa fedha TARI imepanga kujenga maabara moja ya kuzalisha miche kwa njia ya chupa katika kituo cha TARI Mlingano na kukarabati maabara moja na kununua vifaa na vitendanishi katika kituo cha TARI Mikocheni.
Amesema ujenzi na ukarabati wa maabara hizo utaongeza uzalishaji wa miche kutoka 5,131,835 hadi 33,500,000 kwa njia ya chupa.
Amebainisha kuwa TARI imepanga kuboresha maabara ya udongo katika kituo cha TARI Mlingano ili iweze kupata ithibati ya kimataifa.
“Tumepanga kununua magari 35, matrekta 10 na zana zake; na mashine tano (5) za kuchakata mbegu kwa vituo vya TARI Seliani, TARI Ilonga, TARI Uyole, TARI Hombolo na TARI Tumbi ambapo Matreka hayo yataoneza eneo la mashamba ya kuzalisha mbegu kutoka hekta 285 hadi hekta 854,”amesema Dk.Richard Kasuga
MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI
Katika kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji Dk.Kasuga alisema wizara ya Kilimo imeitengea TARI fedha za kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika eneo la hekta 854 kwenye vituo 15 vya utafiti wa kilimo.
Amesema miundombinu hiyo itakayojengwa ni pamoja na mifereji, mabwawa katika kituo cha Ilonga na Tumbi, kuchimba visima, kununua vifaa vya kumwagilia kuchimba mitaro na kutandaza mabomba.
Aidha Dk.Richard Kasuga amesema kuwa TARI itaenda pamoja na ujenzi wa ghala tano zenye uwezo wa kuhifadhi tani 415 za mbegu kila moja yatakayojengwa katika vituo vya TARI Makutupora, TARI Seliani, TARI Hombolo, TARI Kifyulilo na TARI Dakawa.
“Ujenzi huo ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi mbegu kutoka tani 20 za sasa hadi tani 2,075 kwa vituo hivyo. Vilevile, ghala tano za kuhifadhi mbegu zitakarabatiwa katika vituo vya TARI Uyole tatu na TARI Ilonga mbili,”amesema Dk.Richard Kasuga
Dk.Kasuga amesema shughuli zinazotekelezwa na TARI zinachangia katika utekelezaji a Ajenda 10/30 inayosisitiza kilimo ni biashara, na kwamba ifikapo mwaka 2030 kilimo kiwe kinakua kwa asilimia 10.
Amesema shughuli za utafiti na uzalishaji wa Mbegu bora ni miongoni mwa vipaumbele vya juu ambavyo TARI inahusika kuvitekeleza ili kufikia AJENDA 10/30.