Na Thobias Mwanakatwe
MBUNGE wa Jimbo la Songwe, Mhe. Philip Mulugo, ameahidi kutoa Sh.330,000
kila mwezi kwa ajili ya kuwalipa mshahara walimu 11 wanaojitolea katika Shule
ya Sekondari ya Namalaji iliyopo kata ya Totowe wilaya hapa.
Aidha, Mhe. Mulugo ameahidi kutoa Sh.milioni 3 mwezi Novemba mwaka huu kwa
ajili ya kununulia photocopy mashine ambayo itasaidia walimu wakati wanapotunga
mitihani.
Mulugo alichukua uamuzi huo baada ya kutembelea shule hiyo na kuelezwa na
wanafunzi kuwa shule hiyo ina walimu watatu tu walioajiriwa na serikali lakini
walimu 11 wanafundishi kwa kujitolea.
Wanafunzi hao walimweleza Mhe.Mulugo kuwa walimu hao wanaojitolea wamekuwa
wakilipwa kwa wazazi kuchangishana Sh.6,000 lakini hata hivyo baadhi hawatoi fedha hizo.
Kufuatia hali hiyo, Mhe. Mulugo alisema ataanza kutoa Sh.330,000 kila mwezi
kulipa mshahara walimu hao wanaojitolea wakati wanasubiri ajira kutoka
serikalini.
Alisema fedha hizo atakuwa akizituma kila mwezi kwa diwani wa kata ya
Totowe ambaye naye ataziwasilisha kwa Mkuu wa Shule hiyo na yeye kuwagawia walimu hao.