Home Michezo DKT.LAWRENCE GAMA ALIVYOPACHA KUMBUKUMBU ZINAZOISHI RUVUMA

DKT.LAWRENCE GAMA ALIVYOPACHA KUMBUKUMBU ZINAZOISHI RUVUMA

0

HAYATI Dkt.Lawrence Gama ni miongoni mwa viongozi wachache nchini ambao wananchi na watanzania kwa ujumla hawataweza kuwasahau kutokana na kufanyakazi ambazo zinaendelea kuishi licha ya kutangulia mbele ya haki.

Dkt. Gama anaendelea kuishi mkoani Ruvuma kutokana na kuacha kumbukumbu nyingi ambazo zinaendelea kuishi huku baadhi ya wananchi wakimtaja kuwa ni kiongozi ambaye kamwe hawataweza kumsahau.

Uchunguzi umebaini kuwa Hayati Dkt.Lawrence Gama  atakumbukwa sana kwa utaratibu wake wa Utendaji kazi wa kuunganisha nguvu za pamoja, kuthamini utu,mahusiano kazini,kupiga vita majungu na fitina kazini. 

Waliofanya naye kazi wanasema,Dkt.Gama alichukia umaskini kwa wananchi ndiyo maana alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma  kuanzia mwaka 1977 hadi 1987 alianzisha Agizo la Mlale.

Agizo hili ndio lilikuwa kichocheo cha  kusukuma maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma katika Nyanja za kilimo cha kisasa, nyumba bora za tofali za Kuchoma na kuezekwa kwa mabati,kujenga Uwanja wa majimaji na  kuanzisha Klabu cha Soka ya Majimaji ambayo ilichukua ubingwa wa Muungano mara mbili.

Katika kipindi ambacho Dkt.Gama aliwatumikia wananchi wa Mkoa wa Ruvuma,ulifanyika ujenzi wa Barabara ya  lami kutoka Makambako hadi Songea hivyo kumaliza changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa barabara ya lami.

Dkt.Lawrence Gama akiwa madarakani aliendesha Kampeni ya Kuondoa Njaa Tunduru (KUNJATU),pia Dkt.Gama ni Mwanzilishi wa Makumbusho ya Mashujaa wa Majimaji iliyojengwa mwaka 1980 Mahenge mjini Songea ambayo tangu mwaka 2010 imepandishwa hadhi na kuwa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.

Kumbukumbu nyingi zimeachwa na Hayati Dkt.Gama ikiwemo Ujenzi wa Soko kuu la Songea  Baada ya soko la zamani kuungua kwa moto.

Marehemu Dkt.Gama alizaliwa Januari 19,1935  katika kijiji cha Chiulungi Peramiho Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, akiwa ni mtoto wa Pili kwa Nduna Adam Mtazama Gama kwa mama Veronica Mlangeni.

Historia ya Dkt.Gama inaonesha kuwa alisoma katika Shule za Msingi Magagura na Peramiho darasa la kwanza hadi la nane na kisha kujiunga na shule ya sekondari ya Wavulana Ndanda  wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Mafunzo aliyowahi kuchukua ni pamoja na ,Cheti cha Sheria Chuo kikuu cha Dar es salaam,Shahada ya Uzamili (Master of Arts) Siasa na Uchumi) Berlin nchini Ujerumani na Shahada ya udaktari (Phd) Siasa na Uchumi)  Berlin nchini Ujerumani.

Historia ya Dkt.Gama inaonesha kuwa wakati wa uhai wake alipata mafunzo kazini sehemu mbalimbali yakiwemo mafunzo ya ngazi ya juu JWTZ,mafunzo ya uongozi wa Vijana nchini Israeli,mafunzo ya Usalama nchini Uingereza, Romania na China na mafunzo ya juu ya Menejimenti Washington DC nchini Marekani na Ireland.

Dkt.Gama wakati wa uhai wake amewahi kufanya kazi mbalimbali zikiwemo Mkaguzi Msaidizi Idara ya kazi (Labour Inspection) na katika Jeshi la Polisi  alikuwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Bukoba na Ukerewe.

Hayati Dkt.Gama aliteuliwa kati ya maafisa wa chache wa Jeshi la Polisi kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa ambapo baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Jeshi la Kujenga Taifa,kisha aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Historia ya Hayati Dkt. Gama inaonesha kuwa mwaka1975 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma  ambao alitumikia hadi mwaka 1987.

Kwa mujibu wa historia hiyo,Mwaka 1989 Hayati Dkt.Gama aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora,mwaka 1993 Aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM na mwaka 1995 Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambapo kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Songea Mjini.

Watanzania wengi hasa wanamichezo,wataendelea kumkumbuka Hayati Dkt.Gama kama mwanamichezo mahiri aliyependa soka,ukiacha ujenzi wa uwanja wa Majimaji na kuanzisha timu ya Majimaji mkoani Ruvuma,kumbukumbu nyingine alizoacha ni ujenzi wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na Kuanzishwa timu ya Soka  Milambo FC.

Dkt.Gama Alifariki  Desemba 13 mwaka 2008 katika Hospitali ya Aghakhan jijini Dar es salaam na kuzikwa kijijini kwake Amani Makoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma,ameacha Mjane, watoto 14, wajukuu 22 na vilembwe kadhaa.

Hakuna ubishi Dkt.Lawrence Gama ataendelea kukumbukwa kwa sababu kazi alizosimamia zinaendelea kuishi na kuwanufaisha watanzania wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.

Imeandikwa na Albano Midelo

Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini mkoani Ruvuma

Mei 23,2022