******************
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imewapatia mafunzo Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA), kulinda afya zao pamoja na kuangalia mienendo ya maisha yao ya kila siku ili kuepuka magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo na kufanya afya ya akili kuwa imara.
Mafunzo hayo yametolewa Mei 14,2022 katika Ukumbi wa PSSSF Jijini Dar es Salaam ambapo yalitolewa na wataalam wa afya na akiki kutika TACAIDS.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mtalamu wa Saikolojia kutoka Psychologist BRICH Innovation Associate. Bi. Violeth Ndosi ameeleza kuwa karibia asilimia 50 ya msongo wa mawazo unatokea mahali pa kazi na hii ni kutokana na watumishi kutotimiza wajibu wao na kutokujali muda.
Ameongeza kuwa ni vizuri kila mmoja akawa balozi wa maisha yake katika kujali afya, kujali watu wanaomzunguka, kujali kazi na nafasi yake kazini kwani yote haya yakitimizwa yatasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kufanya afya ya akili kuwa imara.
“Maisha ya sasa yamebadilika kutokana na utandawazi kwani watu wanajali sana shughuli zao na kukosa muda wa kukaa karibu na familia zao”.Amesema
Amefafanua kuwa kutokana na hali hiyo malezi ya watoto yamekuwa ni changamoto na kusababisha vijana wengi kuathirika kisaikolojia kutokana na mazingira wanayoishi.
“Sasa hivi kumekuwepo na ongezeko la wavuta bangi, mashoga, wanaojiuza pamoja na vibaka jambo ambalo si jema kwa ustawi wa jamii na ndiyo chanzo kimojawapo cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI,”alifafanua Bi. Ndosi.
Pia Bi. Ndosi amewataka watumishi kutenga muda kwa ajili ya mazoezi pamoja na kuzingatia mlo kamili wa kila siku ili kuwa na afya bora.
Mwakilishi wa Mratibu wa Kudhibiti VVU katika Taasisi za Umma kutoka TACAIDS, Dkt. Patrick Kanyamwenge akiwasilisha mada kuhusu magonjwa sugu yasiyoambukiza amesema kuwa yapo magonjwa mengi sugu yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiathiri mwenendo wa maisha ya kila siku, hivyo ni vyema watumishi wakitambua afya zao mapema na kuweka mipango madhubuti ya kuhakikisha Afya zao zinaendelea kuwa imara.
Dkt. Kanyamwenge ametoa ufafanuzi wa aina mbalimbali ya magonjwa yasiyoambukiza yanavyoathiri watu wengi na kusababisha hata kuharibu mfumo wa maisha yao kiujumla.
Aidha Dkt. Kanyamwenge ameeleza kuwa magonjwa haya yamekuwa yakiathiri sana mfumo wa maisha na kusababisha wengi kutofikia malengo pamoja na ndoto zao ambayo ni pamoja na kisukari, moyo, figo, saratani na mengine mengi.
Pamoja na hayo amewataka watumishi wa BRELA kupima afya zao mara kwa mara na kuzingatia mienendo ya maisha yao ya kila siku, ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa.
Akifunga mafunzo haya ya siku moja, Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji Bw. Daimon Kisyombe amemshukuru Dkt. Kanyamwenge pamoja na Bi. Ndosi kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa kwa kuthamini afya za watumishi kwa kuwapatia elimu juu ya VVU, UKIMWI,magonjwa sugu yasiyoambukiza na Afya ya Akili mahala pa kazi.