Na Alex Sonna-DODOMA
Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuharakisha upitishaji wa maandiko ya miradi ya kimkakati ya Halmashauri ili kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo kwa wakati.
Chikota ameyasema hayo leo April 14,2022 jijini Dodoma wakati akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka 2022/23.
Amesema kuna tatizo la kucheleweshwa kwa maandiko ya miradi ya Halmashauri katika Ofisi hiyo na kwamba hadi sasa asilimia 32 za fedha ndio zimetolewa.
“Asilimia 32 ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya kimkakati ndio zimetumika ina maana maandiko hayapitiswi kwa wakati, maandiko mengine yanahitaji maamuzi ya muda mchache.”
“Nikupe mfano Mamlaka za Serikali za Mitaa za Lindi na Mtwara wengi wameomba kujenga maghala ya kuhifadhi korosho kutokana na mikoa hiyo kulima korosho, zingepewa fedha wangerejesha kwa haraka kwasababu kwa mjengeko wa bei kilo moja ya korosho inalipwa Sh.38, Halmashauri za Mkoa wa Mtwara zimezalisha tani 178 kuna takribani Sh.Bilioni tano zingepatikana hata wakienda kukopa benki za kibiashara uwezekano wa kurudisha kwa muda mfupi upo”
Amesema andiko la aina hiyo halina sababu ya kukaa muda mrefu kila msimu wa korosho wanunuzi wanahitaji maghala.
“Tupunguze Halmashauri kutegemea serikali kuu tungeruhusu halmashauri hizi kujenga maghala kwa kuwa takribani kila Halmashauri ingepata Sh.Milioni 500 kila mwaka,”amesema.