Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango akizungumza katika uzinduzi wa tawi la Meru benki ya CRDB uliofanyika mjini Arusha.
Afisa Mkuu wa uendeshaji benki ya CRDB , Bruce Mwile akizungumza katika uzinduzi huo iliofanyika Jijini Arusha.
………………………………………………
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Mkuu wa wilaya ya Arumeru , Mhandisi Richard Ruyango amewataka wajasiriamali wadogo nchini kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na benki ya CRDB ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto mbalimbali.
Akizungumza katika uzinduzi wa tawi la benki ya CRDB Meru,uliofanyika mjini Arusha,amesema kundi la wajasiriamali wadogo limekuwa likisahaulika sana na Taasisi za kibenki.
“Wajasiriamali wengi hukosa dhamana hivyo wanakuwa hawakopesheki kirahisi jambo limefanyiwa kazi sasa kuna fursa kwa wajasiriamali kupata mikopo benki” amesema.
Hata hivyo ameitaka benki hiyo kulegeza na kuboresha masharti ya upatikanaji wa mikopo ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi ambao wana uhitaji mkubwa wa mikopo huku wakiogopa kiwango kikubwa cha riba kinachotozwa na baadhi ya mabenki.
Ameitaka benki hiyo kujikita katika utoaji wa elimu juu ya umuhimu na huduma za kibenki ili wananchi wengi zaidi waweze kujua umuhimu wa kuweka fedha zao kwani kuna wananchi ambao bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu faida za benki.
Naye Afisa Mkuu wa uendeshaji benki ya CRDB ,Bruce Mwile amesema kuwa,kwa upande wa mkoa wa Arusha benki hiyo inatoa huduma kupitia matawi 16 ambapo matawi 7 yapo mjini huku wakitoa huduma kupitia CRDB wakala ambapo katika wilaya ya Arusha wana jumla ya wakala 1,423.
Ameongeza kuwa ,katika ufunguzi wa tawi hilo la benki hiyo ya CRDB Meru limekuwa likitoa huduma za kawaida kwa wateja wote,hivyo kutokana na kuongezeka mahitaji ya wateja ,ikaona umuhimu wa kuboresha huduma za tawi hilo ili kuendana na mahitaji yaliyopo Sasa na ya baadaye .
“baada ya benki kufanya utafiti wa kina,benki ilifanya maamuzi ya kuboresha jengo kwa kuongeza nafasi kwa ajili ya kuhudumia wateja wengi zaidi , pamoja na kuanzisha huduma kwa ajili ya wateja maalumu “Premier Centre”ambayo haikuwepo katika tawi hilo hapo awali”amesema.
Ameongeza kuwa, benki hiyo imekuwa ikitoa huduma za uwezeshaji kupitia mikopo ikiwemo mikopo binafsi kwa ajili ya wafanyakazi na wastaafu wa sekta ya umma na binafsi ambayo hivi karibuni wamepunguza riba kutoka asilimia 16 hadi asilimia 20 hadi asilimia 9,pamoja na mikopo ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ambapo wamejikita zaidi katika mikopo kwa kundi la wajasiriamali .
Naye Kaimu Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya kaskazini ,David Peter amesema kuwa, benki hiyo ina jumla ya matawi makubwa 41 Kanda ya kaskazini huku ikiwa na ATM 98 na wafanyakazi 300 ,ambapo wameboresha huduma zao kwa lengo la kuwahudumia wateja wengi zaidi