MWENYEKITI wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) Dk.Paul Loisulie,akizungumzia mafanikio ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ndani ya mwaka mmoja.
…………………………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), kimetaja mambo saba ambayo yamefanywa ya serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ndani ya mwaka mmoja ikiwamo upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wanaostahili.
Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk.Paul Loisulie ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwaka mmoja wa Rais Samia kwa wafanyakazi hao.
Dk.Loisulie amesema Rais Samia ameondoa mateso ya Bodi ya Mikopo uliowatesa wafanyakazi kwa miaka kadhaa kwa kuondoa tozo ya kutunza thamani ya mkopo ambayo ilikuwa inaongeza mkopo kila mwaka badala ya kupunguza.
Amesema kiburi cha madaraka kwa wakuu na watendaji wa taasisi kimepungua, kuongezeka kwa amani na utulivu ofisini mwa wafanyakazi kutokana na mabadiliko hayo.
“Awali, wafanyakazi wengi walikuwa katika hali ya uoga na njia panda kutokana na vitisho, pia kufufuka kwa matumaini ya maboresho ya mishahara iliyosimamishwa kupandishwa kwa miaka mitano iliyotangulia, hii ni baada ya kutoa ahadi ya kuboresha maslahi ya mishahara katika sherehe za Mei Mosi jijini Mwanza mwaka 2021,”amesema.
Dk.Loisulie amesema kuendelea kulipwa malimbikizo ya mishahara na maslahi mengine kwa awamu mbalimbali na kuongeza kwa umri wa wanufaika wa Bima ya Afya kutoka miaka 18 hadi 21.
MATARAJIO YAJAYO
Mwenyekiti huyo amesema wafanyakazi wana matumaini makubwa na Rais Samia atazitafutia ufumbuzi kero zao ambazo wameziwasilisha kwa maandishi kwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi mwishoni mwa mwaka 2021.
“Katika andiko hilo tulilowasilisha, tulichambua kwa kina kila suala kwa kuonesha chanzo chake, madhara, namna ya kutatua na tija itakayopatikana baada ya kutatuliwa, baadhi ya masuala hayo ni malalamiko juu ya marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma kuhusu muda wa kustaafu watumishi wanataaluma,”amesema.
Amesema malalamiko yaliyojitokeza kwa watumishi wa Umma yanayolenga Waraka wa Msajili wa Hazina namba sita wa mwaka 2015 ambao unaleta athari kubwa kwa mishahara ya wafanyakazi waendeshaji wa mkondo wa PGSS.
“Kukosekana kwa Sheria ya Kazi na miongozo ya serikali inayoweka viwango vya mishahara katika sekta binafsi ya Taasisi za Elimu ya Juu, Masuala yaliyobakia kupatiwa ufumbuzi katika Bodi ya Mikopo likiwemo suala la ushirikishaji wa vyama vya wafanyakazi kwenye Bodi ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi Elimu ya Juu (HESLB) na mengine machache,”amesema.
Pia ametaja mambo mengine ni ucheleweshwaji wa mafao kwa waastaafu, kukosekana kwa fao la huduma ya afya baada ya kustaafu na kusitishwa kwa nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa watumishi.
“Pia mabadiliko ya Sheria ya Utumishi wa Umma ambayo inaleta athari kwa taratibu za nidhamu kwa watumishi wa umma kwa sababu ya matumizi mabaya,”amesema.
Kuhusu nyongeza ya mishahara, Mwenyekiti huyo amesema ilikwama kwa miaka sita sasa na wana matumaini lipo ndani ya uwezo wa Rais Samia kutokana na kauli aliyoitoa mwaka jana wakati wa sherehe za Mei Mosi mkoani Mwanza kwamba ambapo aliahidi nyongeza kwa mwaka huu.
“Sisi wafanyakazi kwa tunaunganisha nguvu zetu za sala na dua kwa Mama ili aweze kutafuna fupa hili sugu,Tunaamini liko ndani ya uwezo wake na Mungu yupo pamoja nae, zipo faida nyingi za kuongeza mishahara kwa wafanyakazi kijamii, kisiasa na kiuchumi,”amesema.