Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko (kushoto) akimsikiliza mjasiriamali anayetengeneza sabuni wakati alipotembelea maonesho ya wanawake wajasiriamali leo yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) jijini Dar es Salaam. Mkemia Mkuu wa Serikali (wa tatu kutoka kulia) akiwa pamoja na viongozi na wafanyakazi wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) alipotembelea maonesho ya wajasiriamali wanawake jijini Dar es Salaam.
************************
Na Fatma Salum-GCLA
Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amewahimiza wajasiriamali kuzingatia matumizi salama ya kemikali wanazotumia katika uzalishaji wa bidhaa zao ili kulinda afya za binadamu na mazingira.
Dkt. Mafumiko ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea maonesho ya wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ambayo yanafanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.
Aliwaeleza wajasiriamali hao kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika utekelezaji wa majukumu yake imekuwa ikitoa mafunzo kuhusu matumizi salama ya kemikali kwa wadau wake mbalimbali wanaotumia kemikali wakiwemo wajasiriamali ili kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali pamoja na namna bora ya kuhifadhi bidhaa zao.
“Kwa nafasi yetu kama wasimamizi wa sheria ya kemikali tuna jukumu la kuhakikisha watumiaji wa kemikali kama vile watengeneza batiki na wanaosindika bidhaa za vyakula pamoja na dawa asili wanazingatia taratibu za kiusalama, hivyo tunawaahidi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wadau hao,” alisisitiza Dkt. Mafumiko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila alisema kuwa katika zoezi la kuwafikia wajasiriamali, taasisi yake inapata ushirikiano mzuri kutoka GCLA kwenye kuwaelimisha wajasiriamali hao namna bora na salama ya kutumia kemikali katika uzalishaji wa bidhaa.
Aidha, baadhi ya wajasiriamali waliowahi kupata mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kutoka GCLA walieleza kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kuboresha bidhaa zao na kulinda afya zao bila kuchafua mazingira.
Naye mjasiriamali kutoka Zanzibar, Salma Othman ameiomba GCLA iendelee kutoa elimu kwa wadau wengi zaidi kupitia njia mbalimbali ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inazingatia usalama wa afya za watu na mazingira.
Maonesho hayo ya pili ya wajasiriamali wanawake yaliyoandaliwa na TWCC yalianza Machi 3 mwaka huu na yanatarajiwa kukamilika Machi 8, 2022 ambayo ni Siku ya Wanawake Duniani.