Mbunge wa
Kisesa, Luhaga Mpina akizungumza bungeni Jijini Dodoma
BUNGE
limehitimisha rasmi Mkutano wake wa 6 Kikao cha 14 mjini Dodoma huku sakata la
kukatika kwa umeme pamoja na kusuasua kwa ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kuzalisha
umeme la Julius Nyerere kuteka mkutano huo.
Baadhi
ya wabunge Wakichangia taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu za Kamati za
Bunge za Bajeti, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Kamati ya Bunge
ya Nishati na Madini na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) bungeni jijini
Dodoma walielezea kutoridhishwa kwako na tatizo la umeme linavyowatesa wananchi
na kusuasua kwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Wabunge
hao ni pamoja na Mbunge wa Jimbo Mkinga Mkoa wa Tanga, Mhe. Dunstan Luka Kitandula
, Mbunge wa Jimbo Nyasa , Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Injinia Stella Martin Manyanya,
Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Mkoa wa Geita, Mhe. Joseph Kasheku Msukuma,
Mbunge wa Jimbo la Igalula Mkoa wa Tabora, Mhe. Venant Daud Protas, Mbunge wa
Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Mhe. Jesca David
Kishoa.
Mbunge
wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina amewaonya baadhi ya Mawaziri
kuacha kumuhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan katika udhaifu wao wa kiutendaji huku akiwataka kuwajibika kikamilifu
katika wizara zao.
Pia
Mpina amemuomba Spika wa Bunge kuunda Kamati Teule ya Bunge ili pamoja na mambo
mengine ichunguze kwa kina chanzo na sababu za kukatikakatika na mgao wa umeme
unaondelea, kuchunguza kwa kina uwezo wa Bodi na Menejimenti ya TANESCO katika
kuliongoza shirika na kupendekeza hatua za kuchukua.
Amesema
pia Kamati hiyo teule ya Bunge pamoja na mambo mengine ichunguze kwa kina
sababu na chanzo cha kusuasua kwa ujenzi wa mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme
la Mwalimu Julius Nyerere na kupendekeza hatua za kuchukua ili kunusuru mradi
huu mkubwa.
Mpina
amesema Katakata ya umeme inayoendelea nchini hivi sasa imeleta madhara makubwa
ikiwemo kupotea kwa ajira za watanzania, kushuka kwa uzalishaji viwandani,
mfumko mkubwa wa bei, kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi, mapato ya Serikali
kushuka na uchumi kuyumba, lakini pia inarudisha nyuma jitihada nzuri na kubwa
anazofanya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za
kuvutia wawekezaji kuja nchini.
Ameongeza
kuwa sababu zinazotolewa za kukatikakatika kwa umeme zinazua maswali mengi
ambapo Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na majibu ya Waziri wa
Nishati yaliyotolewa bungeni kwa nyakati tofauti yanaleta mkanganyiko mkubwa na
yanakinzana na kuleta hofu kubwa kwa watanzania wanaotegemea nishati ya umeme kuendesha
maisha yao.
Mpina
amesema ni siku chache pia alihoji bungeni sababu za katakata na mgao wa umeme
unaoendelea nchini ambapo Waziri wa Nishati alieleza kuwa inatokana na
matengenezo makubwa ya mitambo ya kufua
umeme na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme.
Amesema
pia kwa nyakati tofauti Waziri wa Nishati
alieleza kuwa watu waliwahi kutishiwa kufukuzwa kwa kukata umeme kwa
ajili ya kufanya Scheduled repairs wakaacha scheduled repairs kwa miaka mitano
kwa kuogopa kufukuzwa.
“Wakati
huo huo tena Serikali ilisema sababu za katakata ya umeme zinasababishwa na
kupungua kwa maji katika mabwawa ya kufua umeme kulikosababishwa na ukame”
alihoji Mpina
Aidha
Mpina amesema pia TANESCO mara kadhaa ilikanusha kuwepo kwa mgao wa umeme wakati
maeneo mbalimbali nchini yakiwa hayana nishati ya uhakika ya umeme na shughuli
na biashara nyingi zinasuasua.
Alisema
TANESCO ikaja tena na kutangaza mgao wa siku 10 wa kuanzia saa 2 asubuhi hadi
saa 6 usiku na baadae tena yakatolewa maelezo kuwa mgao hautakuwa na makali
kama ulivyotangazwa kwa kuwa shirika limefanya tathmini ya uhitaji.
Mpina
amesema suala la matengenezo ya mitambo na miundombinu linaelezwa kiujumla
jumla sana, haielezwi ni mitambo gani na miundombinu gani ambayo haikufanyiwa
matengenezo kwa miaka sita iliyopita na ikaweza kuendelea kufanya kazi bila
umeme kukatika katika kipindi chote hicho.
“Je
kitalaamu inawezekanaje mitambo na miundombinu ya umeme isiyofanyiwa
matengenezo kwa ratiba iliyowekwa (scheduled Maintenance) na umeme ukaendelea
kuwaka kama kawaida?” amehoji Mpina.
Mpina
amesema mapato ya TANESCO yamezidi kuongezeka kutoka Tsh. Bilioni 72 kwa
mwezi mwaka 2015 hadi kufikia Tsh. Bilioni
160 kwa mwezi mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 102, pia katika kipindi
cha mwaka 2019/2020 TANESCO ilipata faida ya Tsh Bilioni 45.25. TANESCO imeacha
kutegemea ruzuku kutoka serikalini ya kiasi cha Tsh. Bilioni 143 huku mapato
yakifikia Tsh. Trilioni 2.4 mwaka 2021.
Aidha
amesema pia mitambo ya kukodi ya kufua umeme kwa kutumia mafuta ya IPTL,
Aggreko na Symbion ilizimwa na hivyo kupelekea TANESCO kuokoa hasara ya kiasi cha Tsh Bilioni 719 kwa mwaka.
Pia
TANESCO ilifanikiwa kuanza kununua vifaa vya umeme ndani ya nchi kama nguzo,
transfoma, nyaya na mita za Luku hali ambayo ilipelekea kuokoa kiasi cha Tsh
Bilioni 162.23 kwa mwaka huku madeni sugu ya TANESCO yakipungua kutoka Tsh
Bilioni 272 hadi Tsh. Bilioni 49.
Hivyo amesema kwa ongezeko hilo kubwa la mapato ya
TANESCO na kwa kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinalipwa kwenye mikataba mibovu
suala la ukosefu wa fedha za matengenezo linatoka wapi.
Mpina amehoji kuwa Waziri wa Nishati ameeleza kuwa
ukarabati na matengenezo ulikuwa haufanyiki kikamilifu kutokana na fedha kidogo
zilizokuwa zikitengwa na TANESCO katika bajeti (Repair and Maintenance), je ukarabati
na matengenezo yanayoendelea hivi sasa yanatumia fedha gani kwa kuwa bado tuko
ndani bajeti ya mwaka 2021/2022.
Hata
hivyo, katika kipindi cha miaka 5 kazi kubwa ilifanyika ya kujenga miradi mipya
mikubwa ya kuzalisha umeme, vituo vikubwa vya kupoza umeme (Sub-Stations) na
kukarabati mitambo ya kufua umeme na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza
umeme ambapo ilipelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kutoka Mw 1,309
mwaka 2015 hadi Mw 1,605.86 mwaka 2020. Ongezeko hili limewezesha nchi yetu
kuwa na umeme wa ziada Mw 187.
Pia
usambazaji wa umeme vijijini uliongezeka kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015 hadi
kufikia vijiji 10,312 mwaka 2020 na idadi ya watumiaji umeme ikaongezeka kutoka
asilimia 35 mpaka asilimia 85.
Hata
hivyo Mpina amesema ukarabati na matengenezo ya mitambo na miundombinu ya umeme
haifanyiki yote kwa pamoja lakini pia
tuna umeme wa ziada Mw 187 ambao unaruhusu kufanya ukarabati na matengenezo kwa
awamu bila kukata umeme.
“TANESCO
ilikuwa ikifanya kazi zake vizuri licha ya changamoto ilizonazo na hatukuwahi
kuwa na katikakatika ya umeme ya aina hii na sasa yameibuka madai mapya kwamba
hadi TANESCO ipate Trilioni 2 za ukarabati na matengenezo ndio mgao wa umeme
utaisha nchini” amesema Mpina.
Hivyo
amesema kwa kuwa sababu zinazotolewa na Waziri
wa Nishati kuhusu kukatikakatika na mgao wa umeme unaondelea hivi sasa
hazieleweki na zinaleta mkanganyiko na hofu kubwa kwa wananchi wanaotegemea
umeme kuendesha maisha yao.
Na
kwa kuwa, kila inapohojiwa kuhusu tatizo kubwa la umeme nchini Waziri wa
Nishati amekuwa akisema asiandamwe na asishambuliwe binafsi katika suala hili.
“Hivyo
basi Mheshimiwa Naibu Spika kwa heshima na unyenyevu mkubwa nakuomba ukubali
Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liunde Kamati Teule ya
Bunge ili pamoja na mambo mengine Kamati ichunguze kwa kina chanzo na sababu za
kukatikakatika na mgao wa umeme unaondelea, kuchunguza kwa kina uwezo wa Bodi
na Menejimenti ya TANESCO katika kuliongoza shirika na kupendekeza hatua za
kuchukua” aliomba Mpina.
Aidha
kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Julius Nyerere
Megawati 2,115, Mpina amesema Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza
mradi huu utekelezaji wake unasuasua na uko nyuma kwa asilimia 44.13 kulingana
na mpango kazi uliokubalika kimkataba.
Huku
sababu za kuchelewa zikielezwa kuwa ni mkandarasi kushindwa kufuata mpango kazi
wa mradi na mkandarasi kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba.
Mpina
amesema tangu mradi huo ulipoanza kujengwa tarehe 15, Juni 2019 ilipofikia
Mwezi Mei 2021 Serikali na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini zilieleza
kwamba ujenzi wa mradi huu ulikuwa umefikia asilimia 52 na hapakuwa na
changamoto yoyote na wananchi waliahidiwa kuwa kufikia Novemba 15, 2021 maji
yataanza kuingizwa kwenye bwawa bila kukosa ikiwa ni hatua muhimu ya ukamilishaji
wa mradi huo.
Lakini
maelezo ya Waziri wa Nishati kuwa siku ya kwanza anaripoti ofisini Septemba
2021 mradi ulikuwa umechelewa kwa siku 477 inaleta maswali mengi .
Mpina
amesema kufikia Disemba 2021 Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeripoti
kuwa mradi huu umefikia asilimia 53.25 tu ambapo kimkataba ulipaswa kuwa
umefikia asilimia 97.38 ukiwa nyuma ya utekelezaji kwa asilimia 44.13.
“Hii
ina maana kwamba kuna ongezeko la asilimia 1.25
tu katika kipindi chote cha Miezi 7 iliyopita yaani kutoka Mei hadi
Disemba 2021 hii ni ishara kwamba ujenzi wa mradi huu unasuasua na hauwezi
kukamilika tarehe 14 Juni 2022 kama ilivyopangwa kwa mujibu wa mkataba” amesema
Mpina.
Mpina
amesema mradi huo umekuwa ukikaguliwa mara kwa mara na umekuwa ukitembelewa na
viongozi mbalimbali zikiwemo Kamati za Bunge, Viongozi Wakuu wa Kitaifa na
haijawahi kuelezwa kama kuna changamoto yoyote ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba fedha zote zilizohitajika zilitolewa na
Serikali kwa wakati.
Amesema
ilipofika Oktoba 2021 ilielezwa kuwa mkandarasi hataweza kuingiza maji kwenye
bwawa Novemba 15, 2021 kwa kuwa mkandarasi alikaidi kufuata design iliyowekwa
na wataalamu ya kujenga mahandaki matatu ya kuchepusha maji ya Mto Rufiji na
badala yake akajenga handaki moja hali iliyopelekea kuchelewa kukamilisha kazi
hiyo, wakati huo huo sababu zilizowasilishwa na mkandarasi za kusingizia Uviko-
19 zilikataliwa na Serikali.
Mpina
akaongeza kuwa baadaye Serikali ilitoa sababu nyingine zilizopelekea kuchelewa
kuingiza maji kwenye bwawa kufikia Novemba 15, 2021 kuwa ni mkandarasi
kuchelewa kuleta mitambo ya kubebea milango (Hoist Crane System) kutokana na
viwanda kufungwa na safari za meli kuathiriwa na janga la Uviko-19.
Aidha
ameongeza kuwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ililieleza Bunge sababu 9
zilizotolewa na Serikali juu ya kusuasua kwa mradi huo ambazo zote
zimesababishwa na mkandarasi kushindwa kufuata mpango kazi na kutekeleza
masharti ya mkataba lakini jambo la kusikitisha hadi sasa hakuna hatua yoyote
kwa mujibu wa mkataba iliyochukuliwa na Serikali dhidi ya mkandarasi huyo.
Mpina
amesema kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa majibu kinzani kila inapopata nafasi
ya kueleza sababu za kuchelewa kwa ujenzi wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Na
kwa kuwa hakuna hatua yoyote
iliyochukuliwa kwa mkandarasi kwa mujibu wa mkataba hadi sasa licha ya
mradi kuripotiwa kuchelewa kwa asilimia 44.13
“Hivyo
basi naliomba Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liunde
Kamati Teule ili pamoja na mambo mengine kuchunguza kwa kina sababu na chanzo
cha kusuasua ujenzi wa mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius
Nyerere na kupendekeza hatua za kuchukua
ili kunusuru mradi huu mkubwa”amesema Mpina.
Mbali
na suala la umeme, pia Mpina ameitaka Serikali kuijengea uwezo wa kifedha na
rasilimali watu Ofisi ya Msajili wa Hazina ili iweze kutekeleza majukumu yake
kikamilifu ya kuyasimamia Mashirika ya Umma yapatayo 237 ambapo kwa sasa uwezo
wake wa kusimamia ni asilimia 13 tu.
Mpina
amesema ukurasa wa 31 wa Taarifa ya Kamati ya Bajeti jedwali namba 1
linaloonyesha mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambapo mapato yasiyo
ya kodi hadi kufikia Disemba 2021 yalikuwa ni asilimia 36 tu.
“Hapa
Serikali haijaleta mchanganuo wa kila wizara na taasisi na kiasi
kilichokusanywa ili kuliwezesha Bunge kujua ni wizara gani na taasisi gani
iliyoshindwa kukusanya kikamilifu mapato ya Serikali. Makusanyo ya miezi 6 kuwa
asilimia 36 ina maana kuwa hakuna uwezekano wa kufikia asilimia 100 kama
ilivyopangwa, mwaka wa fedha uliopita tulielezwa sababu ya kushindwa kukusanya
mapato ya Serikali ilitokana na athari za janga la Uviko-19, leo tuelezwe
sababu ya kuporomoka kwa mapato yasiyo ya kodi ni nini huku kukiwa hakuna
Corona”amehoji Mpina.
Katika
hatua nyingine Mpina ameeleza kusikitishwa kwake namna ajira za watanzania
zinavyopokwa na wageni katika nchi yetu, ajira za watanzania hazina ulinzi hali
iliyopelekea nguvu kazi ya watanzania wapatao milioni 60 kutoshiriki kikamilifu
katika shughuli za kuleta maendeleo ya nchi yao, huku ajira zao zikichukuliwa
na wageni na wao kubaki watazamaji.
Mpina
amesema iko mifano ya Serikali kununua bidhaa na huduma nje ya nchi hata zile
zinazopatikana nchini mfano Wizara ya Mifugo na Uvuvi mwaka 2021/2022 imeanza
kuagiza dawa za kuogesha mifugo kutoka nje ya nchi wakati kuna viwanda vya
watanzania vilivyoajiri wazawa na vinazalisha dawa hizo kwa wingi na zenye
ubora unaostahili.
Aidha
ametolea mfano mwingine ni ujenzi wa barabara na madaraja kupewa wageni hata
kwa miradi ambayo ingeweza kutekelezwa na wazawa, mfano huko Maswa mkoani
Simiyu barabara ya lami ya kilomita 11 amepewa mkandarasi kutoka nje ya nchi na
mshauri elekezi kutoka nje.
Eneo
lingine ni kitendo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuingia mkataba
Novemba 2021 na Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya India Tech Mahindra wa
Tsh. Bilioni 69 ili kuboresha utoaji huduma kwa mtandao huku nchi yetu ikiwa imepiga
hatua kubwa sana katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA.
“Tuna
vijana wabobezi nchini wa kupigiwa mfano na wamebuni mifumo mingi ikiwemo GePG,
Max Malipo nk. iweje leo washindwe kujenga mfumo utakaowafaa TANESCO haya yote
yanafanyika Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lipo na Serikali ipo” amesema Mpina.