Home Siasa CCM YASISITIZA UTEKELEZAJI WA YOTE YALIOAHIDIWA KWA WANANCHI

CCM YASISITIZA UTEKELEZAJI WA YOTE YALIOAHIDIWA KWA WANANCHI

0

************

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amewahakikishia wanachama na wananchi kwa ujumla kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha, kila kilichoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2020 – 2025, kitatekelezwa kwa kiwango chenye tija.

Katibu Mkuu ameyasema hayo leo Jumatatu, Januari 24, mwaka huu, alipokuwa akizungumza na wananchi na wanaCCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Wilaya za Wete na Micheweni katika ziara maalum ya siku mbili yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kuhamasisha uhai wa chama ngazi za mashina, akiambatana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

“Niwahakikishe Chama Cha Mapinduzi kimejipanga, kitafanya kila linalowezekana kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025 ambayo imeahidi mambo mbalimbali ikiwemo maji, umeme, barabara, miundombinu ya elimu…imeahidi mambo mengi ndani yake, inatekelezwa kwa kiwango chenye tija.”

Akitoa salam na ujumbe wa Viongozi Wakuu wa Serikali, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa wananchi wa wilaya ya Wete , Chongolo amesema kuwa;

“Rais Samia ameniambia niwahakikishie kuwa, ataendelea kushirikiana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kupambana kwa ajili ya miradi na changamoto zinazowakabili ili ndani ya miaka mitano wilaya ya Wete na Pemba kwa ujumla kuwe na mabadiliko makubwa ya maendeleo.”

Aidha, Katibu Mkuu akitoa salama za Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleze kuwa;

“Anajua changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa baadhi ya maeneo ya Wete, na amewahakikisha maji yatawafikia wananchi wote kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 kama ilivyo kwa kijiji cha Taifu kilicho kuwa na uhaba wa maji kwa zaidi ya miaka 14 na sasa maji yanapatikana ya kutosha.”

Aidha katika hatua nyingine Katibu Mkuu akikagua ujenzi wa Hospitali ya Wete amewata wananchi wote kuwa macho kupiita na kukagua miradi ya ujenzi ya hospitali za wilaya unaoendelea katika wilaya zote za Kaskazini Pemba ikiwemo Wilaya ya Wete ambapo zaidi ya shilingi bilioni 4.71 zimeshapelekwa na ujenzi unaendelea.

Akizungumza na wanaCCM na wananchi kwenye Mkutano wa Shina Namba moja, tawi la Kiuyu, Kigongoni, Wilaya ya Wete, ametoa wito kwa wanachama wa CCM wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa ndani wa chama mwaka huu, lazima wajipime na wajue wajibu wa uongozi ndani ya chama ndani na nje ya chama, wasisukumwe na tamaa binafsi kutaka uongozi, bali kutumikia watu.

Pamoja na hayo, Katibu Mkuu amewataka wananchi kuhamasishana na kujiandaa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika  mwaka huu, kwani takwimu ni msingi wa mipango ya maendeleo na usambazaji wa huduma za jamii.

Imetolewa na;

Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)