Home Michezo MAJALIWA: SERIKALI ZA EAC KUENDELEA KUKUZA SEKTA YA MICHEZO

MAJALIWA: SERIKALI ZA EAC KUENDELEA KUKUZA SEKTA YA MICHEZO

0

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua mashindano ya 11 ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Baadhi ya washiriki wa  mashindano ya 11 ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua Mashindano hayo kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha,

Washirki wa Mashidano ya 11 ya Mabuge ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki  wakishangilia wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasili kwenye ukumbi wa Hotelli ya Mount Meru jijini Arusha kufungua Mashindano hayo, Desemba 6, 2021. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………………………………………….

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  zitaendelea kuchukua hatua za makusudi za kukuza michezo ndani ya jumuiya hiyo.

Amesema kuwa hivi sasa, sekta ya michezo imekuwa chanzo kikubwa cha biashara, utalii, kuimarisha afya na ajira kwa vijana.

Amesema hayo leo (Jumatatu, Desemba 06, 2021) wakati wa akifungua mashindano ya 11 ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijini Arusha.

“Nitoe wito tuendelee kutumia majukwaa ya namna hii kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuimarisha ushirikiano wetu kwa ajili ya mustakabali na manufaa makubwa ya wananchi wetu”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa michezo hiyo lengo lake kuu ni kuimarisha mahusiano na kuifanya jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa imara zaidi “Majukwaa ya namna hii yamekuwa chachu ya kuleta mwamko mkubwa wa masuala ya sanaa, burudani na michezo ndani ya jumuiya”

Pia, Waziri Mkuu amewasihi wabunge hao waendelee kuimarisha ushiriki wao kwenye masuala ya michezo kwani imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha afya na hivyo kusaidia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza. “Kwa hiyo, nitoe rai kwa Bunge la Afrika Mashariki kusimamia kwa karibu ushiriki wa michezo kwa wabunge na hata wananchi wa Jumuiya yetu”

Kaulimbiu ya Mashindano hayo ni “Strengthening Integration through Inter-Parliamentary Games in the Covid-19 era” yaani kuimarisha masuala ya mtangamano katika kipindi hiki cha UVIKO-19 kupitia Mashindano ya Mabunge ya Jumuiya.

Awali, Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Martin Ngoga, amesema kuwa moja ya lengo la michezo hiyo ni kujenga mshikamano wa kibunge na kuendeleza mahusiano ya kibunge katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Naibu Spika wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema kama mashindano hayo yatasaidia kuongeza umoja kama nchi za Afrika Mashariki ambao wameamua kuwa wamoja “pamoja na mashindano haya watapata fursa ya kujadiliana na hatimaye kuja ma mambo ambayo tutawashauri viongozi wa nchi zetu juu ya ustawi wa wananchi wetu”

Katibu Mkuu wa Jumuiya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki amesema kuwa michezo hii ni sehemu ya jitihada za Jumuiya hiyo kuiunga mkono Tanzania wakati inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru “mbali na hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuhakikishie kuwa Jumuiya yetu ipo imara na inakuwa kwa kasi sana na hii ni sababu ya ushirikiano tunaoupata kutoka kwa viongozi wa nchi”