Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, akizungumza jana na waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa maulidi na harambee ya kuchangia ununuzi wa kiwanja cha upanuzi wa Msikiti wa Jihad, Nyabusalu, Kiseke wilayani Ilemela.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Massala,akizungumza kabla ya kuendesha harambee ya ununuzi wa kiwanja cha upanuzi wa msikiti wa Jihad Nyabusalu,uliopo Kiseke katika Manispaa ya Ilemela jana.
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, wa nne kutok kushoto akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Kiseke kwa masheikhe kutoka mikoa ya Tabora na Shinyanga baada ya kutembelea mradi huo
Sheikhe Mohamed Mbega , kutoka kushoto wa tatu akizungumza jana kwenye eneo la ujenzi wa kituo cha afya Kiseke,wilayani Ilemela, kinachojengwa kwa nguvu na michango ya Waislamu.Wa nne kutoka kushoto ni Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke.
Masheikhe kutoka katika mikoa ya Shinyanga na Tabora ,jana wakishiriki pamoja na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke (wa pili kutok kulia), kuomba dua kwenye eneo la ujenzi wa kituo cha afya Kiseke kinachojengwa kwa michango ya waislamu bada ya kutembelea mradi huo.Wa kwanza kulia ni Sheikhe Msafiri Kitumbo wa Shinyanga.Picha na Baltazar Mashaka
……………………………………………………
NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,limewataka waumini wa dini ya Kiislamu kuacha kulalamika na kuilaumu serikali, wafanye shughuli za maendeleo,wasisumbuliwe na vyeo (madaraka).
Pia limewataka kusomesha watoto wao na kufanya mambo ya maendeleo badala ya kusubiri hisani ya serikali kwa kuwa yanayofanywa na BAKWATA,madhehebu mengine yametangulia,hivyo wakipuuza watabaki nyuma.
Rai hiyo ilitolewa jana na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke,alipozungumza na waumini wa Msikiti wa Jihad Nyabusalu, Kiseke katika Wilaya ya Ilemela,kwenye Sherehe ya Maulidi ya Mtume Muhammad S.A.W.
Alisema Waislamu wanapaswa kujitambua kwa kuchangia na kufanya maendeleo kwa maslahi yao badala ya kulalamika na kuilaumu serikali.
“Hatuwezi kuwa watu wa kulalamika tu,tufanye maendeleo ya waislamu, haiwezekani serikali ichukue sh. milioni 4 itupe tu, za nini? Tuseme ukweli, serikali itatuunga mkono kama kuna jambo la maendeleo,hivyo tufute mambo ya kulalamika,”alisema Sheikhe Kabeke.
Alitahadharisha Mwanza kuna tatizo kubwa la ushirikiano,kwenye elimu bado hawajaitumika vizuri na kusistiza ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea,waendeleze mshikamano na kusameheana kwani hakuna mkamilifu,”alishauri.
Naye Sheikhe wa Wilaya ya Tabora, Sheikhe Ramadhan Rashid,alimmwagia sifa Sheikhe Kabeke kwa anayoyafanya ni makubwa ili kuchochea maendeleo,hafanyi ili kulinda nafasi yake bali maslahi ya waislamu na kwa jinsi hiyo Mwanza itabadilika na itaendelea kwa sababu hafanyi maigizo kuhamasisha maendeleo.
Mgeni rasmi kwenye maulidi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Massala,alisema lipo jambo la kujifunza kwa Sheikhe Kabeke,amekuwa mwanaharakati wa maendeleo na dini hata serikali inapokwama amekuwa kinara wa kuikwamua kwenye changamoto zinazoikabili likiwemo suala la chanjo ya Uviko-19.
Alisema jamii kupitia kwa kiongozi huyo wa kiroho ilihamasika kuchanja baada ya upotoshaji uliofanywa na watu wasioitakia mema nchi yetu na kuwaomba viongozi wengine wa dini na kisiasa kuendelea kuhamasisha chanjo ya kujikinga na ugonjwa huo na kuwataka waislamu waitumie tunu hiyo, wasiyaone mapungufu bali mazuri yake kwa maslahi mapana ya uislamu.
“Sheikhe Kabeke umefanya kazi kubwa ya kuhamasisha ujenzi wa vituo vya afya,unahisi unawajengea waislamu tu bali Watanzania wote na serikali hatutakuacha pekee yako, tutakuunga mkono kutafuta matofali ya ujenzi huo,binafsi nitakuunga mkono kwenye jambo hili la heri,pia ”alisema Massala.