Home Michezo MASHINDANO YA MBIO ZA MITUMBWI KUFANYIKA DISEMBA 4 UKEREWE

MASHINDANO YA MBIO ZA MITUMBWI KUFANYIKA DISEMBA 4 UKEREWE

0
Washiriki wa mbio za mitumbwi za kupiga makasia wakionyeshana kazi ndani ya Ziwa Victoria kuwania zawadi ya fedha taslimu zaidi ya milioni 10 mwaka huu.Picha na Baltazar Mashaka 

…………………………………………………………….

NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza

MBIO za kupiga makasia maarufu Tanzania Boat Race kwananume na wanawake, zitafanyika kwa nyakati tofauti katika ufukwe wa Monarch wilayani Ukerewe na Kirumba jijini Mwanza.

Mashindano hayo yanayoandaliwa na kampuni ya Scope Solution Ltd,yatafanyika Disemba 4, mwaka huu, kwenye ufukwe wa Monarch, wilayani Ukerewe kabla ya kuhitimishwa katika ufukwe wa soko la Kimtaifa la Samaki la Kirumba Mwaloni,Disemba 12, mwaka huu.

Mratibu wa mbio hizo za mitumbwi,Ayub Sossy, akizungumza na waandishi wa habari jana,alisema zinafanyika kwa jitihada za wadau mbalimbali wakishirikiana na kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Alisema dhamira ya kampuni ya Scope Solution ni kuyafanya mashindano hayo kuwa endelevu, yafanyike kila mwaka yakilenga kuhamasisha na kukuza utalii,kutangaza utamaduni wa Kitanzania na washiriki kunufaika kiuchumi.

“Mashindano haya mbali na kutoa burudani kwa wananchi na kuwanufaisha kiuchumi washiriki kwa zawadi za fedha,tunalenga kutangaza utamaduni,vivutio vya utalii na utalii,elimu kwa jamii kujikinga na magonjwa hatari Malaria,VVU na Ukimwi na tutahamasisha chanjo ya Uviko-19,”alisema Ayubu.

Alisema mwaka huu timu 60 zinatarajiwa kushiriki mbio hizo za makasia, kutoka wilaya za Nyamagana,Misungwi,Ilemela,Sengerema na Magu na watayaboresha na kutanua wigo zaidi mwakani ili kutoa fursa kwa wapiga makasia wa mikoa ya Geita,Kagera,Mara na Simiyu.

Alitoa rai kwa wananchi wa Ukerewe na Jiji la Mwanza,kujitokeza kushuhudia mbio hizo pamoja wavuvi kuandikisha kushiriki mashindano hayo ili kujiongezea kipato ambapo fomu za ushiriki zitatolewa bure kuanzia Disemba 1 hadi 8 kwa washindani wa Mwanza.
Kwa upande wake, Meneja wa TBL wa Mwanza na Geita,Issa Makani, alisema kwa kutambua umuhimu na mashindano ya mitumbwi na fursa za Ziwa Victoria  kiuchumi na kijmii,wameamua kuyadhamini kupitia kinywaji cha Balimi ambapo elimu ya afya itatolewa kutokana na afya kuwa msingi mkuu wa maendeleo.

“Mashindano ya mitumbwi ni fursa ya kuwaleta pamoja wananchi na jamii, ndio maana TBL tumeingiza mikono na furaha yetu ni kuona yanafanikiwa na tutaendelea kuyadhamini,”alisema.

Naye Ofisa Mawasiliano wa Bonde la Ziwa Victoria, Perpetua Masaga,alisema watatumia mbio hizo kutoa elimu na kuhamasisha wananchi na jamii umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na Ziwa Victoria linalotegemewa na mikoa mingi ili kuhakikisha rasilimali hiyo haipotei,ikipotea ni dhahiri hakutafanyika chochote cha kiuchumi na matumizi mengine ya kibinadamu.

Aidha Ofisa Mwandamizi wa Hifadhi ya Saanane, Deogratus Ndelolia, alisema kupitia michezo wanahamasisha utalii wa ndani kwa wananchi na wageni kutembelea hifadhi hiyo iliyopo ndani ya Ziwa Victoria, hivyo washiriki wa mbio za mitumbwi watumie fursa kutembelea vivutio vinavyopatikana Saanane.

Kwa mujibu wa Ayub Julius,timu bingwa ya mbio hizo  kwa Jiji la Mwanza itajinyakulia sh. milioni 2.5,ya pili sh.1.5, timu ya tatu sh.1,000,000,  ya nne 800,000 na itakayoshika nafasi ya tano sh.500,000 huku bingwa kwa Ukerewe akipata sh.1,000,000,mshindi wa pili,800,000 na mshindi wa tatu sh.500,000.