Home Mchanganyiko WAZIRI DK.TAX  ATAJA MAFANIKIO YA WIZARA YA  ULINZI NA JESHI LA KUJENGA...

WAZIRI DK.TAX  ATAJA MAFANIKIO YA WIZARA YA  ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA TANGU UHURU

0

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Stergomena Tax ,akizungumza na waandishi wa habari  leo November 29,2021 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Stergomena Tax (hayupo pichani) wakati akiwasilisha  mafanikio ya Wizara hiyo  katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Stergomena Tax,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na  waandishi wa habari (hawapo pichani)  leo November 29,2021 jijini Dodoma wakati akizungumzia mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.

…………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,imesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara  Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya wanajeshi kote nchini.

Hayo yamesemwa leo  Novemba 29,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Stergomena Tax,  wakati akizungumzia mafanikio ya wizara hiyo  katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.

Dk.Tax amesema kuwa Wizara imetekeleza mradi wa nyumba 6,064 katika mikoa tisa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Kusini Pemba, Pwani na Tanga.Kujengwa kwa nyumba hizo kumeliwezesha Jeshi kupunguza uhaba wa nyumba za kuishi Wanajeshi na Watumishi wa Umma,.

”Ukarabati wa baadhi ya nyumba za zamani pamoja na majengo ya huduma kama vile hospitali, mabwalo, mabweni ya kuishi askari, shule, vyuo na miundombinu mingine umeendelea kufanyika chini ya Wizara.”amesema Dk.Tax

USHIRIKIANO

Wizara kupitia JWTZ imeendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika Operesheni za Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali zenye migogoro kwa kupeleka vikosi, waangalizi wa kijeshi, wanadhimu na makamanda.

Amesema Nchi ambazo JWTZ imewahi kushiriki katika ulinzi wa amani ni Liberia, Eritrea, Shelisheli, Ivory Coast (sasa Cote D’Ivoire), Comoros, Sierra Leone, na Sudan.

“Hivi sasa JWTZ linashiriki Ulinzi wa Amani katika nchi za Lebanon, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji na Sudan Kusini,”amesema.

MIPAKA YA CHIN IPO SALAMA

Waziri Stergomena amesema Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaendelea kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi inaendelea kuwa salama.

“Wito wa Wizara kwa Wananchi ni kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa nchi kwa kujitoa kwa namna itakavyohitajika, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za viashiria vya matishio ya kiulinzi na kiusalama.

“Kama alivyowahi kusema mwasisi wa Taifa hili Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere nanukuu “Jukumu la Ulinzi wa Taifa ni Jukumu la Kila Mwananchi”.Kwa muktadha huu, jukumu la ulinzi si la Wizara pekee bali ni la kila mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yetu, hivyo tuendelee kuwa pamoja kulilinda Taifa letu,”amesema.

VIWANDA NA GAWIO KWA SERIKALI

Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, Serikali imeweza kuanzisha viwanda vya kijeshi ikiwemo pamoja na Tanzania Automotive Technology Centre (TATC), maarufu kama NYUMBU, Shirika la Mzinga na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT).

“Mashirika haya hufanya utafiti na uhawilishaji wa teknolojia, uzalishaji wa vitendea kazi, na bidhaa na huduma mbalimbali kwa matumizi ya kijeshi na kiraia, uzalishaji mali na miradi ya Kimkakati,”amesema.

Aidha, SUMAJKT inaendelea kujenga na kuimarisha viwanda,Kiwanda cha ushonaji Mgulani (National Service Garments Factory).

“Kiwanda hiki kimekuwa mkombozi mkubwa kwa Serikali, hususan katika vyombo vya ulinzi na usalama kwani kimeweza kushona sare mbalimbali za majeshi yetu na kupunguza gharama za ununuzi wa sare kutoka nje ya nchi,”amesema.

Amesema kuanzia mwaka wa fedha 2017/18 SUMAJKT imeweza kutoa gawio kwa Serikali la jumla ya Shilingi billioni 3.78 kutokana na faida inayopatikana katika uzalishaji.

KILIMO

Dk.Tax amesema Wizara kupitia JKT imeendelea pia kutekeleza Mkakati wa Kilimo (2019/2020 – 2024/25) wa kuliwezesha JKT kujitosheleza kwa Chakula. Mkakati huo unatekelezwa katika vikosi vya Chita – Morogoro, Milundikwa – Rukwa, Mlale – Ruvuma, Mgambo – Tanga na Oljoro – Arusha kwa kutumia vyanzo vya ndani vya JKT, na bajeti ya Serikali.

Aidha, Wizara kupitia JKT inashiriki katika kilimo cha mazao ya kimkakati ya Taifa, ambayo ni Michikichi – Bulombora – Kigoma, Mkonge – Maramba na Mgambo Tanga, Korosho – Nachingwea na Manyoni Singida, Alizeti – Makutupora Dodoma, na Kahawa – Itende Mbeya na Tarime – Mara.

“Katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, Wizara kupitia JKT inaendelea na ujenzi wa mfumo wa umwagiliaji (irrigation scheme) katika shamba la Mpunga – Chita, ambalo ni shamba la mfano na limechangia kwa kiasi kikubwa katika kulisha vikosi vya Jeshi na kupunguza utegemezi,”amesema.