Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akifungua kikao cha Wizara ya Maliasili na Wadau wa Malikale wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Allan Kijazi.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Malikale Bw Mwita William akifafanua jambo kwenye kikao cha Wizara ya Maliasili na Wadau wa Malikale wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga Bi Mwantumu Mgonja akizungumza na wanahabari juu ya mikakati yake ya kulinda na kuendeleza Malikale nchini.
Wadau wa Utalii kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wakifatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi kwenye kikao cha wadau wa Malikale wa Ukanda huo wa Pwani.
****************************
Na Sixmund Begashe
Serikali za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani zatakiwa kutambua kuwa urithi wa malikale uliopo katika mikoa hiyo ni budi ulindwe na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho ili Malikale hizo ziendelee kutumika kama zao la utalii na, hivyo kusaidia wananchi waliopo katika maeneo husika kujipatia kipato.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Allan Kijazi kwenye kikao cha wadau wa Malikale wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani ili kujadili ushiriki wa Serikali za Mitaa na wadau katika uhifadhi na uendelezaji wa malikale.
Dkt Kijazi amesema kwa kipindi cha hivi karibuni uhifadhi wa malikale katika nchi nyingi umeendelea kuwa muhimu, kwani umeonekana kuvutia watalii wengi kutembelea maeneo ya kihistoria, palentolojia na akiolojia. Kwa hapa nchini watalii wengi wamekuwa wakitembelea Bonde la Olduvai na Mji Mkongwe wa Zanzibar.
”Katika Bara la Afrika taarifa zinaonesha kuwa Nchi ya Siera Leone imefanikiwa kuendeleza njia na maeneo yanayohusiana na utumwa kama vile mji wa kihistoria wa Bunce ambao upo katika kisiwa cha Bunce kuwa kivutio cha utalii. Kisiwa cha Bunce na mji wake ndilo eneo ambalo miaka 200 iliyopita, watumwa walikuwa wakiondokea kutoka nchini Siera Leone kuelekea Bara la Amerika”. Aliongeza Dkt Kijazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Bw Ramadhani Possi licha ya kuipongeza Wizara kwa kuwakutanisha wadau wa Malikale wa Mikoa ya Pwani, amesema kikao hicho kimekuwa chachu kwao na kuahidi kuendelea kutenga fedha za kutosha ili zitumike kuhakikisha uhifathi endelevu wa maeneo hayo unafanyika na kuvutia watalii wengi kwenye Mbuga ya Sadani yenye historia kubwa.
Nae Afisa Utamaduni Halmashauri ya Bagamoyo Bw Hamisi Kimenya, amesema kuwa Wilaya ya Bagamoyo inautajiri mkubwa wa Malikale hivyo kupitia kikao hicho wao kama Afisa Utamaduni wameongezewa wigo mpana wa uwelewa juu ya umuhimu wa uhifadhi wa maeneo hayo na kuyaendeleza.
Mkurugenzi wa Halmashauri Mkuranga Bi Mwantumu Mgonja nae licha ya kuipongeza Wizara ya Maliasili kwa kikao hicho amesema Halmashauri yake imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha inaunga mkono jitihada za Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano Mama Samiha Suluhu Hasan za kutangaza vivutio vya utalii ambavyo nipamoja na Malikale ili viweze kuwanufaisha wananchi wa Kisarawe na Tanzania kwa Ujumala.
Katika kikao hicho Wizara ya Maliasili na Utalii nchini pamoja na wadau hao wa Malikale kutoka sekta ya Utamaduni na Kurugenzi za Halmashauri za Wilaya za Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamepata nafasi ya kujadili sera za uhifadhi na uendelezaji wa Malikale nchini.