Home Mchanganyiko PROF. MWAKALILA AWATAKA WANAFUNZI MNMA KUJIKITA KWENYE MASOMO

PROF. MWAKALILA AWATAKA WANAFUNZI MNMA KUJIKITA KWENYE MASOMO

0

Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Profesa Shadrack Mwakalila, akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo hicho.

Wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), wakimsikiliza Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila pichani hayupo
*******************************

Na Mwandishi Wetu

MKUU  wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Profesa Shadrack Mwakalila amewataka wanafunzi wa chuo hicho  kujiepusha na masuala ya kisiasa na kuelekeza nguvu kwenye masomo,  ili kupata maarifa bora yatakayowasaidia katika maisha yao na taifa.

Prof Mwakalila ameyasema hayo leo wakati akizungumza na  wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo hicho  na kusisitiza kuwa chuo hicho hakiruhusu itikadi za siasa ndiyo maana wakati wa udahili hakuna mwanafunzi aliyeulizwa chama anachotoka.

Pia aliwaasa wafanyakazi wote wa chuo hicho kutoa huduma bora kwa wanafunzi ili waweze kusoma kwa amani.

“Ili uweze kupata elimu bora lazima mwanafunzi usome kwa juhudi na maarifa, uwe muadilifu na mzalendo, hii itakusaidia wewe na taifa. Pia jiepusheni na makundi ya uchochezi, na mzingatia zaidi masomo pamoja na  kujiepusha na udanganyifu wowote kwenye mitihani,”alisisitiza Prof. Mwakalila.

Pia amewataka wanafunzi hao kulipa ada kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wakati masomo yakiendelea, ikiwa ni pamoja na kujiepusha na tabia za kughushi na kuazimana vitambulisho kwani kufanya hivyo ni kinyume na taraibu na kanuni za chuo.

“Jitahidini kujiepusha na tabia za udanganyifu katika mitihani yenu mkiwa hapa chuoni, kinachotakiwa ni nyinyi kusoma kwa bidi, kujiamini na kushirikiana katika masomo ili mfanye vizuri katika mitihani yenu kwa lengo la kupata  matokeo mazuri,”alisema Prof. Mwakalila.

Prof. Mwakalila pia amewataka  watumishi   wa chuo hicho kutoa huduma zilizobora kwa wanafunzi wote maana wanafunzi ni wateja wao na kwa kufanya hivyo kutawezesha kuwepo kwa  muungano mzuri baina ya wanafunzi na watumishi.

Mkuu huyo wa chuo ameahidi kuwa uongozi wa chuo utahakikisha unaboresha mazingira ya kujifunzia ili kila mwanafunzi aweze kupata maarifa bora na kwa wakati.

Prof Mwakalila amewapongeza kwa kuchaguliwa kujiunga na chuo hicho kinachotoa mafunzo bora katika fani mbalimbali za kitaaluma pamoja na mafunzo maalumu ya uongozi, maadili, utawala bora, uzalendo na utaifa.