Spika wa bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Dokta Martin Ngoga akizungumza katika kongamano hilo jijini Arusha.
Mkurugenzi wa shirika la Crown Trust nchini Kenya , Daisy Amdany  akimkabithi hati hiyo ya maombi ,Spika wa bunge la Jumuiya la Afrika mashariki (EALA) Dokta Martin Ngoga 
Mkurugenzi wa shirika la Crown Trust nchini Kenya ,Daisy Amdany akizungumza katika kongamano hilo jijini Arusha.
……………………………………………………
Happy Lazaro,Arusha.
Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka nchini Kenya   yakiongozwa na shirika la Crown Trust yamemkabithi hati ya maombi  spika wa Bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Mh Martin Ngoga ya kuitaka Kenya kufuata matakwa ya katiba yao kutokana na kutokuwa na theluthi mbili ya wanawake katika uongozi nchini humo kama katiba ya nchi hiyo inavyoelekeza.
Akikabidhi hati hiyo katika kongamano la wanawake bara la Afrika  lililofanyika mkoani Arusha Mkurugenzi wa shirika linalotetea maswala ya wakinamama katika mambo ya siasa,uchumi,na elimu ya umma,(Crown Trust) kutoka nchini Kenya  Daisy Amdany  amesema kuwa Kenya ni nchi ambayo iko mbele kwa Mambo mengi katika jumuiya hiyo lakini imeshindwa  katika masuala ya kuhusisha wanawake Kikatiba katika kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema kuwa, kama mashirika ambayo sio ya kiserikali wameenda mahakamani mara nyingi na wamepewa oda  na mahakama 2020 kuwa  Bunge hilo livunjwe kutokana na kutokuwa na theluthi mbili ya jinsia moja katika uongozi kwani katika nchi zote za jumuiya ni Kenya tuu ndio hawajatekeleza suala hilo.
“Hiyo oda ya mahakama haijatekelezwa na Sasa tuko njiani kuelekea katika uchaguzi mkuu wa tatu chini ya katiba mpya agosti 2022 na hakuna mtu yoyote anayeshughulika na suala hilo ndio maana tunaliomba Bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki kutusaidia kutafuta suluhisho ili Kenya iweze kufuata sheria iliyopo katika katiba yao na isiwache akina mama nyuma,” amesema.
Amefafanua kuwa ,ikiwa Kenya ambaye tayari ni mwenyekiti wa jumuiya ya Afrika Mashariki lakini haishirikishi wanawake ambao ni wengi zaidi  katika nchi hiyo na ikiwa watatengwa Kenya haitilii maanani kuhusisha kwa wanawake katika nyanja za uongozi.
“Uongozi Ni kitu muhimu kwa sababu viongozi ndio wanaotupangia maisha kwani wanapanga bajeti na maendeleo ambayo yatafanyika katika nchi na ikiwa sauti ya akina mama haipo katika hizo meza inamaanisha mambo yetu hakuna na ikiwa Rais wetu na viongozi wanaweza kukataa kukubali Sheria kuu ya nchi ina maanisha ya kwamba hatuko katika hali nzuri tupo kwenye mteremko wa hatari kwani hatuwezi kujua ni Sheria gani nyingine kesho watatupilia mbali,” Amesema.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la jumuiya ya Afrika Mh Martin Ngoga  amesema kuwa, amepokea hati hiyo na ataiwasilisha katika vikao vya Bunge ili kuona ni kwa namna gani wataweza kutafuta suluhu ya jambo ili kuweza kuzifanya nchi wanachana kustawi zaidi na kutokuwa na migogoro.
Aidha   kongamano hilo  limeandaliwa na Mtandao wa  wanawake wa  maendeleo na mawasiliano barani Afrika (FEMNET) kwa kushirikiana na kituo cha usuluhishi (CRC) kwa ufadhili wa shirika la IDEA.