Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (Mb) akizungumza na wadau mbalimbali wa elimu (hawapo pichani) walioshiriki uzinduzi wa mradi wa Jifunze Uelewe uliofanyika mkoani Morogoro katika shule ya msingi Chifu Albert Luthuli.
Mkurugenzi Mkaazi wa shirika la USAID, Kate Somvongsiri akizungumza na wadau mbalimbali wa elimu (hawapo pichani) walioshiriki uzinduzi wa mradi wa Jifunze Uelewe uliofanyika mkoani Morogoro katika shule ya msingi Chifu Albert Luthuli.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro, Germana Mung’aho akizungumza na wadau mbalimbali wa elimu (hawapo pichani) walioshiriki uzinduzi wa mradi wa Jifunze Uelewe uliofanyika mkoani Morogoro katika shule ya msingi Chifu Albert Luthuli.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akiwagawia watoto wasioona kifaa maalum cha kusomea kwa wanafunzi wasioona (braille reader) vinavyotolewa na shirika la USAID wakati wa uzinduzi wa mradi wa Jifunze Uelewe uliofanyika mkoani Morogoro.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akisoma moja ya vitabu vinavyotolewa na shirika la USAID wakati wa uzinduzi wa mradi wa Jifunze Uelewe uliofanyika mkoani Morogoro.
……………………………………………..
#Kuanza na mikoa minne
#Zaidi ya wanafunzi milioni 1.2 na walimu 25,000 kunufaika
Na WyEST,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amezindua mradi wa Jifunze Uelewe wenye lengo la kuboresha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa awali hadi darasa la nne katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Mtwara na Ruvuma wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Uzinduzi wa mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) umefanyika katika shule ya Albert Luthuli mkoani Morogoro ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha utoaji elimu nchini kwa kuhakikisha mazingira salama na jumuishi katika kusoma kwa watoto .
Amesema mradi huo utatoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini 25,578 katika shule 2,825 na kwamba utanufaisha jumla ya wanafunzi 1,259,227 kutoka katika mikoa hiyo.
Aidha, Mhe. Ndalichako ametoa rai kwa wadau wote wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wote nchini wakiwemo wenye mahitaji maalum.
“Niwaombe wadau wote wa elimu, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni binafsi na vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha ushiriki wa pamoja ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum,” amesema Prof. Ndalichako.
Awali, akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la USAID, Kate Somvongsiri amesema mradi wa Jifunze Uelewe utahakikisha wanafunzi wa awali hadi darasa la nne wanapata nyenzo za kujifunzia katika muundo wa machapisho na dijitali ili kuimarisha mtaala na kutoa fursa kwa mazoezi ya kujitegemea.
Amesema mradi utatoa nyenzo za elimu jumuishi ikiwemo vifaa kwa wasioona kama braille readers za kielektroniki, vitabu vya kielektroniki na vifaa vya lugha za alama.
Naye Germana Mung’aho ambaye ni Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huyo, ameishukuru Serikali na Shirika la USAID kwa kuona umuhimu wa kuinua elimu mkoani humo na kuahidi kushirikiana bega kwa bega katika kutekeleza mradi huu ili kufikia malengo yaliyowekwa.