Na Mathias Canal, Wizara
ya Kilimo, Bujumbura-Burundi
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda leo tarehe 18 Octoba
2021 amewasili Mjini Bujumbura nchini Burundi kwa ajili ya ziara ua kikazi ya
siku mbili itakayofanyika tarehe 19-20 Octoba 2021.
Katika ziara hiyo Waziri Mkenda atakutana na kufanya mazungumzo
ya kubadilishana uzoefu na Waziri wa Kilimo wa Burundi kuhusu utekelezaji wa
mifumo ya utoaji ruzuku kwenye pembejeo za Kilimo.
Waziri Mkenda pia anatarajiwa kutembelea kiwanda cha Mbolea cha
FOMI ambacho kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha
mbolea Jijini Dodoma nchini Tanzania na kujadiliana namna ya kuhakikisha ujenzi
na uzalishaji wa kiwanda hicho.
Waziri Mkenda amesema kuwa takribani Asilimia 90 ya mbolea
inaagizwa nje ya nchi hivyo mkakati madhubuti wa serikali ya Tanzania ni
kuhakikisha mbolea inazalishwa nchini ili kuondokana na utegemezi wa uagizaji
wa mbolea nje ya nchi.
Prof Mkenda amesema kuwa Ujenzi wa kiwanda hicho utakapokamilika
kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Tani 600,000 za mbolea ambazo ni Zaidi
ya mahitaji ya mbolea nchini Tanzania ambayo ni kati ya Tani 400,000 mpaka Tani
500,000 kwa mwaka.
Amesema kuwa wakati serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa
kiwanda kikubwa cha mbolea Tanzania lakini serikali inaendelea na mkakati wa
kuhakikisha kuwa inatafuta mbolea inayoweza kupatikana kwa wakati na kuwafikia
wakulima kwa bei nafuu.
Kadhalika, Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda atakutana na
Taasisi za utafiti wa nchini Burundi zinazoshirikiana na kiwanda cha FOMI
katika kufanya tafiti za afya ya udongo na kuibua na kukubaliana maeneo ya
ushirikiano katika kilimo kwa lengo la kukuza uchumi baina ya nchi zote mbili.
Katika ziara hiyo Waziri wa Kilimo ameambatana na Mkurugenzi wa
Mazao wa Wizara ya Kilimo Bw Enock Nyasebwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Mbolea Tanzania Dkt Stephan Ngailo pamoja na mtaalamu wa udongo Dkt Catherine
Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo-TARI Mlingano
kilichopo mkoani Tanga.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amepokelewa na Mwenyeji
wake Bw Salvatory Mbilinyi ambaye ni Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Tanzania
nchini Burundi.