Home Mchanganyiko CHUO KIKUU CHA PORT HARCOURT CHA NCHINI NIGERIA CHAONESHA NIA YA KUFUNDISHA...

CHUO KIKUU CHA PORT HARCOURT CHA NCHINI NIGERIA CHAONESHA NIA YA KUFUNDISHA LUGHA YA KISWAHILI

0

Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayubu Rioba Chacha (kulia) na Mkurugenzi wa Voice of Nigeria Bw. Osita Okechukwu (kushoto) wakiwa na nyaraka baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano jijini Abuja, Nigeria.

Mkutano ukiendelea baina ya Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayubu Rioba Chacha, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana, Maafisa wa Ubalozi na Watendaji wa Nigeria Television Authority (NTA) walipotembelea Taasisi hiyo.

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayubu Rioba Chacha (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria walipotembelea Wizara hiyo.

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (kulia) wakibadilishana nyaraka na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewill.

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (kulia) na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewill wakiwa katika picha ya pamoja.

 ……………………………………………………………..

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Mhe.  Benson Alfred Bana ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Port Harcourt kimeonesha utayari wa kuanza kufundisha tena somo la lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Slaam kama ilivyokuwa awali. 

Balozi Bana amebainisha hayo baada ya kutembelea  na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewillambapo pamoja na masuala mengine walijadili kuhusu uwezekano na namna ya kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika Chuo hicho.

“Taratibu zimeanza kufanyika ili kukamilisha makubaliano ambayo yatapelekea somo la Kiswahili kufundishwa chuoni hapo, hii itatoa fursa kwa Walimu wa Kiswahili wa Tanzania kufundisha somo hilo katika chuo hicho, pia ni fusa muhimu katika kukuza lugha ya Kiswahili ambayo ni sehemu ya Utamaduni wa Mtanzania” Amesema Balozi Bana.

 

Miongo minne iliyopita Chuo kikuu cha Port Harcourt kilikuwa kikifundisha somo la Lugha ya Kiswahili. Hata hivyo kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi, Chuo hicho hakikuendelea kufundisha somo hilo. 

Wakati huohuo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Taasisi ya vyombo vya Habari vya Serikali ya Shirikisho la Nigeria (inayojulikiana kama Voice of Nigeria-VON) wameingia makubaliano ya kukuza lugha Kiswahili nchini humo.  

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa TBC Dkt. Ayubu Rioba Chaha aliyofanya nchini Nigeria ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa VON Bw. Osita Okechukwu. Katika mazungumzo hayo TBC ilikubali kushirikiana na VON kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili VON katika uandaaji na utangazaji wa vipindi vya Kiswahili ikiwemo kubadilishana program, wataalamu na ujuzi katika sekta ya utangazaji.

Mbali na kutembelea VON Dkt. Ayubu Rioba Chacha akiambatana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana na Maafisa wengine wa Ubalozi pia alitembelea; Federal Radio Cooperation of Nigeria (FRCN), Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria na Nigeria Television Authority (NTA)

VON tayari ina kipindi maalumu kinachoendeshwa kwa lugha ya Kiswahili ambacho kilianzishwa mwaka 1969 na iliyokuwa Federal Radio Corporation of Nigeria (FRCN). Matangazo kwa lugha ya Kiswahili yalianzishwa ili kuwafikia wasikilizaji wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini wakati wa juhudi za kupigania ukombozi wa Afrika.