Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas A. Nyamanga wakikabidhiana zawadi baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa ukanda wa nchi
za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya. ——————————————-Sekta
zaidi nchini kunufaika na mikopo nafuu ya Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya
(European Investment Bank-EIB) imekubali kuongeza kasi na wigo wa maeneo ya ushirikiano
baina ya Tanzania na Benki hiyo. Hayo yameelezwa wakati wa mazungumzo baina ya Balozi
wa Tanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas A.
Nyamanga na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa benki
hiyo, Bw. Diederick Zambon yaliyofanyika hivi karibuni kwenye Ubalozi wa
Tanzania, Brussels. Katika
mazungumzo hayo, wawili hao walijadili kwa kina juu ya miradi mbalimbali na fursa
nyingine zinazoweza kunufaisha Tanzania kupitia mikopo nafuu inayotolewa na Benki
hiyo. Miongoni mwa miradi iliyojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa awamu ya pili ya
mradi wa kuboresha msongo mkubwa wa umeme katika vituo vya Iringa na Shinyanga
(Tanzania Electricity Backboneinterconnector project-TBIP II. EIB ilikuwa ni moja
ya taasisi za fedha zilizotoa mkopo nafuu kwa ajili ya mradi huu kwa awamu ya
kwanza (TBIP I). Katika mazungumzo hayo, Bw. Zambon ameonesha utayari wa kuendeleza
mazungumzo zaidi na Serikali ya Tanzania kuhusu mradi huu na miradi mingine ikiwemo
miradi ya maji. Wawili
hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi kwenye utekelezaji wa mradi wa ukarabati
wa viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga na Kigoma pamoja na ujenzi wa uwanja
mpya wa ndege wa Sumbawanga. Mradi huu pia unafadhiliwa na Benki ya EIB kwa mkopo
nafuu wa Euro milioni 50. Benki hiyo
yenye makao yake makuu nchini Luxembourg pia imekubali kuanza majadiliano na Serikali
ya Tanzania pamoja na sekta binafsi ili kukubaliana juu ya mazingira yatakayoiwezesha
Benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa sekta binafsi ili kuchochea zaidi maendeleo
ya Watanzania. Mikopo hiyo italenga zaidi wajasiriamali wadogo na wakati; wakulima
na watanzania wenye viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo;
taasisi mbalimbali za fedha na wafanyabiashara kwa ujumla. Ujumbe
wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Bw. Zambon unatarajiwa kufanya
ziara nchini Tanzania mwezi huu wa Oktoba au mwanzoni mwa Mwezi Novemba mwaka huu
kwa ajili ya kuendeleza majadiliano na Serikali pamoja na sekta binafsi kwenye masuala
haya muhimu kwa uchumi wa Tanzania. EIB ni
miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na imekuwa ikishirikiana na
Serikali na sekta binafsi katika utoaji wa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali nchini. |