Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA) Mhandisi Godfrey Chibulunje,akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 5,2021 jijini Dodoma (hawapo pichani) wakati  akitangaza bei mpya za mafuta kwa Mwezi Oktoba ambazo zitaanza kutozwa kuanzia kesho Oktoba 6, mwaka huu pamoja na  kupunguza Tozo nane.

Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Nishati na Maji  (EWURA) Mhandisi Godfrey Chibulunje (hayupo pichani)  wakati  akitangaza bei mpya za mafuta kwa Mwezi Oktoba ambazo zitaanza kutozwa kuanzia kesho Oktoba 6, mwaka huu pamoja na  kupunguza Tozo nane.

…………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma.

Kufuatia Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan la kuitaka Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA) kuangalia upya bei Pamoja na Tozo,Mamlaka hiyo imetangaza kupunguza Tozo nane kwa ajili ya udhibiti wa EWURA na kuwaletea Unafuu wananchi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 5,2021 jijini Dodoma Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Godfrey Chibulunje,amesema wamefanya marekebisho ya tozo mbalimbali.

Amesema kuwa  tozo hizo ni pamoja na  matumizi ya miundombinu  ya bandari,Mamlaka ya Mapato Tanzania,Wakala wa vipimo Tanzania,pamoja na kupunguza gharama za kuweka vinasaba kwenye mafuta kutoka shilingi 14 kwa lita hadi shilingi saba.

Mhandisi Chibulunje amesema Serikali imebadilisha tozo ya matumizi ya miundombinu ya bandari ambayo inatozwa kwa Dola za Marekani (USD 10MT +VAT) kwa tani na sasa itatozwa kwa shilingi ya Tanzania.

“Na pia tozo hiyo itapunguzwa kufika shilingi 15 kwa lita kutoka wastani wa shilingi 22 kwa lita na kuondoa VAT  katika tozo hii,Mabadiliko haya yataleta  kwa watumiaji  mafuta kwa wastani wa shilingi bilioni 23.15 kwa mwaka  kutokana na matumizi  ya lita bilioni 3.42 kwa takwimu za mwaka 2020,”amesema.

Vilevile,amesema Serikali imepunguza tozo ya TRA ya kuchakata nyaraka  kutoka shilingi 4.8 kwa lita  na kuwa kiwango maalum  cha shilingi milioni 20 kwa kila meli ambapo kwa wastani meli saba huleta shehena ya mafuta kila mwezi.

Pia,Serikali imepunguza tozo ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kwa shilingi moja kwa lita  na kuwa tozo ya kiwango maalum ambacho ni shilingi milioni 7 kwa kila meli baada ya kutozwa kwa kila lita.

“Serikali imepunguza tozo ya TBS ya kupima ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini kutoka shilingi shilingi milioni 1.24 kwa lita na kutozwa kwa kiwango maalum ambacho ni shilingi milioni 12.8,”amesema.

Pia,amesema Serikali imepunguza gharama za kuweka vinasaba kwenye mafuta kutoka shilingi 14 kwa lita hadi shilingi 7 kwa lita.

“Serikali imefuta tozo ya huduma(Service Levy ) inayotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa  kwa Halmashauri za Temeke na Kigamboni kwa Dar es salaam  na Tanga na Mtwara  kwa wafanyabiashara wa jumla  ambao wana maghala ya kuhifadhia  mafuta ya jumla,”amesema

Katika hatua nyingine,Mhanisi Chibulunje  ametaja imetaja bei mpya za mafuta ya Petroll,Dizeli na Mafuta ya taa kuanzia kesho  Oktoba 6 mwaka 2021.

Amesema Dar es salaam Petroli itauzwa sh. 2,439,Dizeli sh.2,261 na Mafuta ya Taa 2,188,Dodoma  Petroll 2,497,Dizeli 2,320 na Mafuta ya Ta ash.2,246.

Mikoa mingine,Arusha Petroll sh.2,535,Dizeli sh.2,301 na mafuta ya ta ash.2,272,Mwanza Petroll sh.2,469,Dizeli sh.2411 na mafuta ya taa sh.2,338.