Home Mchanganyiko MKURUGENZI MKUU WA TEA AASA WANAFUNZI KUJITUMA KATIKA MASOMO

MKURUGENZI MKUU WA TEA AASA WANAFUNZI KUJITUMA KATIKA MASOMO

0

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi Bahati Geuzye Akikabidhi zawadi kwa mmoja wa  wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Makete Wasichana kutokana na kufanya vizuri kitaaluma

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi Bahati Geuzye Akikabidhi zawadi kwa mmoja wa  walimu wa Shule ya Sekondari Makete Wasichana kutokana na kufanikisha wanafunzi kitaaluma

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi Bahati Geuzye (wa kwanza Kushoto) katika hafla ya mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Makete ambako alikuwa Mgeni Rasmi.

Sehemu ya nyumba sita zilizofadhiliwa na Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa ajili ya makazi ya Walimu wa Shule ya Sekodari ya Makete Wasichana

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi Bahati Geuzye (aliyevaa Suti ya Bluu) akifurahia jambo mara baada ya kukagua nyumba sita za walimu wa Shule ya Sekondari Makete Wasichana ambazo zimefadhiliwa na Mfuko wa Elimu wa Taifa  unaosimamiwa na TEA.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makete Wasichana wakimpokea Mgeni Rasmi wa Mahafali ya Pili ya Kidato cha nne, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Bi Bahati Geuzye

*****************************

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi Bahati Geuzye amewahimiza wanafunzi  kujituma  na kuweka bidii katika masomo ili kufikia malengo yao ya kitaaluma.

Ametoa rai hiyo katika mahafali ya pili ya Shule ya Sekondari Makete Wasichana iliyoko Mkoa wa Njombe ambako alikuwa Mgeni Rasmi. Jumla ya wanafunzi 41 wanahitimu kidato cha nne katika shule hiyo.

“Ni lazima kila mmoja wenu awe na maono ya muda mrefu ya kile anachotaka kufanikisha katika maisha yake. Hampaswi kusoma tu kwa mazoea badala yake muweke mipango mikakati katika masomo yanayohusiana na taaluma  mnazozipenda” alisisitiza Bi Geuzye.

Amewakumbusha wanafunzi  hao  wa Shule ya Sekondari Makete Wasichana kuweka kipaumbele katika masomo na kuepuka vishawishi akitoa mfano viongozi na wanataaluma wa kike wamefika hapo walipo kutokana na kuweka kipaumbele katika masomo. “Mfano dhahiri ni Nchi yetu ya Tanzania kuongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa ni Rais wa kwanza mwanamke Tanzania. Ni jambo la kujivunia na kujifunza kuhusu faida za elimu kwa mtoto wa kike.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TEA alikagua nyumba sita za walimu zilizojengwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa, unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu  ambapo aliridhishwa na ubora wake.

Uongozi wa Shule ya Sekondari Makete Wasichana wameishukuru Serikali kwa ufadhili wa ujenzi wa nyumba hizo sita  ambazo zimewapa walimu makazi  yenye hadhi.  Aidha wamepongeza uamuzi wa Serikali wa kuwapa ufadhili wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa. Ujenzi wa nyumba za walimu umegharimu Shilingi Milioni 150 wakati  ufadhili wa madarasa matatu unagharimu Shilingi Milioni 60.

Katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 jumla ya Shilingi Bilioni 8.2 zimetumika kugharimia miradi 199 ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kote nchini. Katika Mkoa wa Njombe TEA imewezesha utekelezaji wa miradi miwili (2) yenye thamani ya Shilingi Milioni 120.