Home Mchanganyiko TWCC YATOA MAFUNZO YA UZALISHAJI WA BIDHAA ZENYE UBORA NA VIWANGO KWA...

TWCC YATOA MAFUNZO YA UZALISHAJI WA BIDHAA ZENYE UBORA NA VIWANGO KWA WAJASIRIAMALI WANAWAKE MKOA WA NJOMBE

0

*******************************

NJOMBE

Kufuatia bidhaa nyingi zinazozalishwa nchini kuzuiliwa kuingia sokoni na mamlaka mbalimbali za ukaguzi nchini ,Chama cha wanawake wafanyabiashara Tanzania(TWCC) kinachofanya kazi ya kuwajengea uwezo kiuchumi wanawake kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kimekusanya akina mama wajasiriamali kutoka halmashauri 6 za mkoa wa Njombe na kisha kutoa elimu ya uzalishaji na ufungaji wa bidhaa zao kwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa katika soko la dunia.

Katika mafunzo hayo ya siku mbili kwa vitendo ambayo yamekutanisha akina mama wajasiamali,TWCC na taasisi tano za serikali ikiwemo TBS,SIDO,WMA na Mkemia mkuu wa serikli yamejikita katika kujenga uelewa na ujuzi wa uzalishaji wa bidhaa zenye viwango vya kimataifa ,hatua ambayo imekuja baada ya chama hicho kufanya utafiti na kubaini kiwango kikubwa cha bidhaa zinazozalishwa na akina mama zinakataliwa sokoni na mamlaka za ukaguzi kutokana na kukosa sifa

Mwajuma Hamza ambaye ni mkurugenzi TWCC amesema ili kufungua milango ya soko la ndani nje wameamua kuzunguka Tanzania bara na Visiwani kuelimisha wanawake wajasiriamali kuzingatia viwango na ubora wa kimataifa wa bidhaa.

“Tumebaini akina mama wengi wanaojihusisha na ujasiriamali wamekuwa na wakati mgumu sokoni kwasababu ya kuzalisha bidhaa ambazo zinakosa sifa hivyo kupitia mafunzo haya watakwenda kupiga hatua na kuuza hadi nje ya nchi” Alisema mkurugenzi wa TWCC Mwajuma Hamza.

Katika mafunzo hayo yaliohudhuriwa na katibu tawala wa mkoa wa Njombe Judica Omary ambaye ndiye aliyefungua mafunzo amesema serikali imeona jitihada kubwa zinafanywa na wanawake katika ujasiriamali ili  kujikwamua kimaisha na kwamba ili kufanikisha maono yao imekuwa ikitoa mikopo ya asilimia 10 kupitia halmashauri .

Katika hatua nyingine Bi Omary amesema changamoto ya masoko serikali itaendelea kuyatafuta huku nguvu kubwa pia ikiwekwa kwenye ubora na viwango vya bidhaa zinazozalishwa ili kukidhi mahitaji ya soko la dunia kwasasa.

Nae Ruth Msafiri aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Njombe ambaye mapema baada ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo aliamua kusalia mjini Njombe na kisha kujikita katika shughuli za ujasiriamali na kilimo huku akisema matarajio yake ni kuja kuwa mzalishaji mkubwa wa maziwa na bata mzinga na kisha baadae kuja kumiliki kiwanda chake cha kuongeza thamani ya bidhaa za maziwa.

Aidha katika mafunzo hayo kumehudhuriwa na afisa vipimo mkuu nchini Gasper Matiku ambaye anasema wamelazimika kufika mkoani Njombe na kisha kutoa elimu ya vipimo kwa wajasiriamali wanazalisha bidhaa mbalimbali ili waweze kuendana na matakwa ya soko la ndani na nje ya Tanzania.

” Kumekuwa na changamoto kubwa sana vipimo katika bidhaa zinazozalishwa nchini hivyo kupitia elimu kama hizi wazalishaji wanapata uelewa wa nini kifanyike ili kuwa na bidhaa bora na zenye viwango vya kidunia sokoni” Alisema Gasper Matiku afisa vipimo mkuu.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Ales Lugenge,Genovefa Barnabas ambaye ni mkurugenzi wa TWCC nyanda za juu kusini wanasema elimu walioipata inakwenda kufungua mipaka ya bidhaa zao sokoni na kwamba wanategemea kwenda kuuza zaidi kwasababu watakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye viwango vya juu.