Home Michezo MAKUMBUSHO YA TAIFA YAIPAMBA  SIMBA DAY

MAKUMBUSHO YA TAIFA YAIPAMBA  SIMBA DAY

0
Na Sixmund J. Begashe
Makumbusho  ya Taifa nchini imeshiriki kwenye siku maalum ya timu ya  Simba kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kwa njia ya kutoa elimu kwa mashabiki wa timu hiyo kuhusu huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Akizungumzia ushiriki huo, Mratibu msaidizi wa Mashirikiano kati ya Timu ya Simba na Makumbusho ya Taifa Bw Edgar Chatanda amesema lengo lao ni kuisogeza Taasisi hiyo kwa Wananchi ili waweze kufahamu majukumu ya msingi na huduma wanazozitoa.
Bw Chatanda ameongeza kuwa safari hii wameongeza wigo wa ushiriki wao ukilinganisha na mwaka jana ambapo walishiriki zaidi kama wageni watazamaji lakini sasa wameweza kuwa na eneo maalumu la kugawa vipeperushi, kuelezea, kujibu maswali ya watu na hata kupokea maoni ya mashabiki hao waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo.
“Kwa niaba ya Makumbusho ya Taifa niupongeze uwongozi, wanachama na wapenzi wa Simba kwa siku yao hii muhimu, pia niushukuru uwongozi huo kwa kuendeleza mashirikiano na Taasisi yetu ambayo kimsingi ni Taasisi ya Watanzania ambao Wanasimba ni sehemu yao” Aliongeza Bw Chatanda
Bw Chatanda alisema tena kuwa moja ya malengo ya Taasisi yao ni kushirikiana na wadau mbalimbali katika shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa urithi wa Utamaduni na Malikale nchini, hivyo wanaendeleza mazungumzo ya mashirikiano na timu zingine za mpira nchini.
Shabiki mmoja wa timu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi ambaye hakutaka jina lake liandikwe licha ya kuipongeza Makumbusho ya Taifa kwa kushiriki katika siku yao kwa kuwapatia elimu muhimu juu ya urithi uliohifadhiwa katika Makumbusho nchini, ameupongeza uongozi wa Club yake kwa mashikiriano hayo na hasa kuwatembeza wachezaji wao Makumbusho hali inayo imarisha uzalendo zaidi kwa wachezaji wa timu hiyo.
Katika kusherekea siku yao maalumu Viongozi, Wachezaji, Washabiki na wapenzi wa Simba wanashudia kikosi kipya cha timu hiyo ambacho kimekutana na timu ya TP Mazembe kutoka DR Congo ambayo imeifunga Simba goli 1-0