Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali mara baada ya tukio la Uapisho lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. PICHA NA IKULU
*******************************
Na Redempta Ndubuja
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuwapanga upya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga bila kutumia nguvu ili wafanye biashara zao kwa kufuata taratibu zilizowekewa .
Amesema hayo leo katika hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua jana tarehe 12 Septemba katika viwanja vya Ikulu jijini Dodoma.
“Serikali ilitoa fursa kubwa kwa machinga kufanya biashara za kujipatia kipato kwa uhuru lakini msitumie fursa hiyo vibaya na kufanya biashara kiholela ambapo baadhi yao hupanga bidhaa nje ya maduka na kuwazuia wenye maduka kufanya biashara , kitendo ambacho kinakosesha kodi toka kwa wafanyabiashara hao,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amewataka viongozi aliowapisha na walio katika nafasi mbalimbali za uongozi kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kuwa mabadiliko aliyofanya katika Baraza la Mawaziri ni yakawaida lakini ni endelevu .
Vilevile, Rais Samia amewataka watendaji Serikalini kuendesha shughuli zao kwa vitendo ili kuwaletea wananchi maendeleo na si kwa maneno makali ambayo hayana tija kwa maendeleo ya wananchi.
Mwisho