*************************
Na.Elisa Shunda, Kigoma.
KATIBU mkuu wa umoja wa wazazi Tanzania jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Gilbert Kalima, amewasisitiza wazazi nchi nzima kuwawekezea watoto wao katika elimu ili kuendelea kupata viongozi wa baadae.
Aliyasema hayo katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi, Ndugu Kalima, katika ziara yake ya kikazi wakati akisalimiana na wanachama wa CCM na jumuiya zake katika wilaya ya Buhigwe, Kasulu na Kibondo.
“Ndugu zangu wananchi wa Mkatanga hapa Buhigwe nawapongeza kwa kupata Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango, anayetokea wilayani hapa na viongozi wengine kadha wa kadha ombi langu kwenu wazazi wangu tuwawekezee elimu vijana wetu ili tuendelee kutengeneza viongozi wajao;
“kama hiyo haitoshi ninafahamu kwamba wananchi katika eneo la mkatanga wameanza kujenga zahanati kwa nguvu zao wenyewe, nami nitafuatilia pamoja na viongozi tuone serikali imefikia wapi katika kuchangia ujenzi huo, natambua ujenzi wa sekondari ya mwaluo ambapo serikali imetoa sh.milioni 63 ni wajibu wenu wananchi na serikali kuisimamia fedha hiyo itumike kama ilivyopangwa”, alisema Kalima.
Akiwa wilayani Kibondo katika kijiji cha Mabamba, katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi, Kalima, alienda kutoa pole nyumbani kwa Mzee Mihira Joel aliyefiwa na mwanae Abeid Joel ambaye alikuwa katibu wa Chadema jimbo la Buhigwe.
Aidha katibu mkuu wa jumuiya ya wazazi, Ndugu Kalima, akiwa wilayani Kibondo, aliwaasa wanachama wa CCM na jumuiya zake kushikamana na kuongeza maradufu upendo katika kipindi hiki wanachoelekea uchaguzi wa ndani wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwakani kwa kuwataka kuchagua viongozi bora na si bora kiongozi.
Aidha Katibu mkuu huyo, Ndugu Kalima, amechangia mifuko ya simenti 20 ambapo 10 ameielekeza katika ujenzi wa zahanati ya mkatanga na mifuko mingine 10 ameielekeza kwenye ujenzi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Buhigwe.
Aidha Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Ndugu, Kalima, kwenye msafara wake ameongozana na Mkuu wa kitengo cha Milki kutoka Makao Makuu ya CCM, William Obimbo na Mwanasheria wa jumuiya ya wazazi taifa, Ndugu Wakili Beatus Mafuru.