WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi cha kufahamiana na Wawakilishi na Wahariri wa vyombo vya habari waliopo Dodoma kilichofanyika leo September 9,2021 jijijni Dodoma.
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,akimsikiliza Mkurugenzi wa Manunuzi Dkt.Christopher Nditi kutoka Wizara ya Maji wakati wa kikao kazi cha kufahamiana na Wawakilishi na Wahariri wa vyombo vya habari waliopo Dodoma kilichofanyika leo September 9,2021 jijijni Dodoma
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,akimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Maji RUWASA Mhandisi Mkama Bwire wakati wa kikao kazi cha kufahamiana na Wawakilishi na Wahariri wa vyombo vya habari waliopo Dodoma kilichofanyika leo September 9,2021 jijijni Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DUWASA),akielezea walivyojipanga kutoa huduma wakati wa kikao cha Waziri wa Maji Jumaa Aweso,alipokutana na Wawakilishi na Wahariri wa vyombo vya habari waliopo Dodoma kilichofanyika leo September 9,2021 jijijni Dodoma
Baadhi ya Wawakilishi na Wahariri wa vyombo vya habari waliopo Dodoma wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha kufahamiana na kilichofanyika leo September 9,2021 jijijni Dodoma.
………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kiasi cha shilingi Bilioni 207 kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa maji Vijijini.
Hayo ameyasema leo September 9,2021 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na Wawakilishi na Wahariri wa vyombo vya habari wenye lengo la kutoa shukurani kwa vyombo hivyo jinsi wanavyoshirikiana na Wizara hiyo na kupelekea kupatikana kwa mafanikio mbalimbali.
Aidha Aweso amesema kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya maji nchini,kwa nia njema Rais Samia katika Bunge la Bajeti ameidhinisha Bilioni 680 kwa Wizara hiyo ili kwenda kutekeleza miradi ya maji mijini na vijijini na kutatua kero ya maji.
Hatua hii imekuja huku Wizara hiyo ikiwa katika mkakati wa kuhakikisha inafikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini huku ikipata fedha Zaidi ya dola milioni 500 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi Tirion moja iliyotokana na mahusisano mazuri kati ya Tanzania na Serikali ya India kupitia Exim Bank.
Aweso ameeleza kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi ya Maji katika miji 28 na kwamba vibali tayari vimepatikana na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni hali itakayosaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.
“Mojawapo ya Miji hiyo ni Makambako,Wanying’ombe,Muheza,Handeni na maeneo mengine ili kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji ya watanzania mijini na vijijini”amesema.
Licha ya hayo ameeleza kuwa katika maeneo ya Vijijini kupitia fedha zilizoidhinishwa na Bunge pamoja na zilizoongezwa na Rais Samia ,Wizara kwa kushirikiana na wakala wa maji vijijini (RUWASA)itaendelea kutoa maelekezo mahsusi kwa wahandisi wote wa maji kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata maelekeo ya wizara hiyo ili kutatua kero ya maji.
Hata hivyo Aweso,ameeleza kuwa ili kuhakikisha Wizara hiyo inafanikiwa kuingia asilimi 85 ya upatikanaji wa maji Vijijini ,kwa mwaka huu imepanga kuingia mikataba 1176 kwa ajili ya kuhakikisha wanajenga miradi ya maji vijijini kwa kuzingatia kuwatumia wakandarasi wenye uwezo.
“Tumezingatia Wakandarasi wasio na uwezo hawatapata miradi,wakandarasi wazuri wanafahamika na wakwamishaji wanafahamika,moja ya changamoto ya ukwamishaji wa miradi ya maji ni wakandarasi wababaishaji wasio na uwezo hatuwezi kuwapa nafasi kwenye wizara yetu,”ameeleza.
Aweso amewataka Wakandarasi walioingia mikataba na Wizara hiyo kulichukulia suala la maji kama vita mahususi ya kuhakikisha watanzania waishio vijijini wanaondokana na kero ya maji na kuwa na uhakika wa kupata maji wakati wote.
Aidha amewataka Wakuu wa Mikoa,Wabunge,Wilaya ,Madiwani na Viongozi wengine kwenda kusimamia miradi ya maji nchini.
“Si busara hata kidogo kuona leo mradi wa maji unakwamishwa kwa kukosa fedha kwa ajili ya ubadhilifu,tunataka wananchi wapate manufaa kutokana na serikali yao hakuna usiri wowote kwenye miradi hii ya maji,tunataka kila kitu kiwe wazi,”amesisitiza Aweso
Pia amesema kuwa upatikanaji wa Maji kwa Jiji la Dodoma ambapo ameeleza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa maji ambapo uwezo wa uzalishaji wa maji kwa sasa ni lita milioni 66 huku mahitaji yakiwa ni lita 103 kutokana na ongezeko la watu.
“Zipo jitihada ambazo wizara hiyo imefanya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma(DUWASA) kwa kuchimba visima maeneo ya pembezoni na kuongeza tenki kubwa eneo la Buigiri ili kuhakikisha maeneo ya Soko la Ndugai,Nzuguni,Njedengwa yanapata maji ifikapo mwezi wa kumi mwaka huu,”amesema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Maji RUWASA Mhandisi Mkama Bwire ,amesema tangu wakala huo uanze kutoa huduma mwaka 2019 , wastani wa upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ilikuwa 64.7 % hadi kufikia mwaka huu Juni ni 72.3% na malengo yao ni kufikia 85% ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amewatoa wasiwasi wakazi wa Jiji la Dodoma kuwa Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya maji itahakikisha inatatua kero zote za maji kwa kufanikisha miradi yote ambayo inaendelea kutekelezwa.
”Tumechimba visima vitano vya ziada pale Ihumwa na tumelaza bomba lenye kilomita 11.6 kutoka Ihumwa kuja Njedengwa ili kuhakikisha maeneo ya pembezoni yanapata maji kupitia visima’’ amesema Mhandis Josph