Mwenyekeiti wa Chama Cha ADATADEA Juma Ali Khatib, akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kuunga mkono kauli ya msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi kwa kuwataka Viongozi wa Vyama vya Siasa kukaa pamoja na Jeshi la Polisi na kufanya mazungumzo, hafla iliyofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekeiti wa Chama cha ADATADEA Juma Ali Khatib akizungumza kuhusu kuunga mkono kauli ya msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Picha Na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar
…………………………………………………………
Na Ali Issa – Maelezo
Mwenyekiti wa chama cha ADATADEA, Juma Ali Khatib ameunga mkono kauli ya msajili wa vyama vya siasa nchini, ya kuvitaka vyama vya siasa kukaa pamoja na jeshi la polisi na kufanya mazungumzo ili kufikia makubaliano.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa sanaa Rahaleo Mjini Unguja, amesema anaunga mkono kauli ya Jaji Francis Mutungi ya kukaa pamoja na jeshi la polisi na kufanya mazungumzo ya kuafikiana kuhusu ufanyaji wa mikutano.
Alisema nchi ya Tanzania ina amani na utulivu hivyo si vyema kusababisha mivutano na jeshi la polisi, jambo ambalo halikubaliki kuona linatokea.
Alieleza kuwa, Msajili mkuu wa vyama vya siasa amekuwa na moyo safi na thabiti, wa kuwaeleza viongozi wa vyama vya siasa kuwa, wakae meza moja na Jeshi la polisi ili kupitisha maamuzi yalio sahihi na kuepukana na mivutano kati yao juu ya kuzuiliwa kufanya mikutano.
“Jaji Fransic Mutungi maneno aliyo yasema kuwaambia viongozi wa vyama vya siasa ni maneno mazuri kabisa, kwani yanajenga umoja, sasa anapotokea kiongozi akalipinga neno hilo na kutaka kuleta uvunjifu wa amani sisi TADEA Hatukubaliani nae”, alisema Mwenyekiti huyo.
Alifahamisha kuwa, njia nzuri ya kupata mustakabali mzuri kati yao na Serikali ni kukubali kukaa na Jeshi hilo ili kuzungumza kwa pamoja, kwa lengo la kufikia makubaliano.
Aidha mwenyekikti huyo aliwaasa wananchi wa vyama vya siasa, kuachana na baadhi ya watu wanao taka kuleta migogoro katika nchi, na kuwataka kudumisha amani iliopo.