Home Mchanganyiko MSAJILI VYAMA VYA SIASA ATOA UFAFANUZI KUHUSU MKUTANO WAKE NA WAANDISHI

MSAJILI VYAMA VYA SIASA ATOA UFAFANUZI KUHUSU MKUTANO WAKE NA WAANDISHI

0

Nachukua fursa hii kutoa ufafanuzi mdogo wa mkutano wangu na waandishi wa habari uliofanyika jana tarehe 06 Septemba, 2021 kwenye ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar-es-salaam. Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, nilieleza kinagaubaga/bayana azma yangu ya kuitisha kikao maalum cha wadau wa tasnia ya siasa kutafuta suluhu ya sintofahamu/mivutano iliyojitokeza baina ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa hususani vyama vinapotaka kufanya makongamano, mikutano ya ndani nk. 

Kwa masikitiko nimebaini baadhi ya wadau kwa sababu wanazozijua wao aidha kwa makusudi au kwa kutokuelewa vizuri wamepotosha taarifa hiyo kwa kudai kuwa nimetoa amri ya kusitisha mikutano ya ndani ya vyama vya siasa. Hilo halina ukweli wowote na niwasihi mlipuuze kwa uzito unaostahili. 

Kimsingi, sijatoa amri ya kuzuia bali nimevishauri vyama vya siasa katika kipindi ambacho tunajaribu kupata ufumbuzi wa mivutano hiyo, ni busara tu ya kawaida kwamba, wakati jitihada zikiendelea vyama vijizuie kwa muda kuendelea na shughuli zilizosababisha kutokea kwa mivutano hiyo. 

Nitoe wito kwa wadau wote wa tasnia ya siasa nchini kuendelea kuwa wastahamilivu wakati jitihada ikiendelea kuwezesha kikao hicho muhimu kufanyika mapema sana iwezekanavyo ili kupata ufumbuzi utakaokuwa wa kudumu na tija kwa pande zote. 

Mungu Ibariki Tanzania. 

Jaft Francisis. K. Mutungi MSAJILI WA WAMA VYA SIASA