Home Mchanganyiko TASAF YAANZA UJENZI WA UKUMBI KATIKA SHEHIA YA KIZIMKAZI UTAKAOWEZESHA WANAFUNZI KUFANYA...

TASAF YAANZA UJENZI WA UKUMBI KATIKA SHEHIA YA KIZIMKAZI UTAKAOWEZESHA WANAFUNZI KUFANYA MITIHANI NA SHUGHULI ZA KIJAMII

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza kuhusu mradi wa ujenzi wa ukumbi wa kufanyia mitihani na shughuli za kijamii mara baada ya ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa mradi huo unaogharamiwa na TASAF katika Shehia ya Kizimkazi Dimbani iliyopo Wilaya ya Kusini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea maelezo ya ujenzi wa mradi wa ukumbi wa kufanyia mitihani na shughuli za kijamii unaogharamiwa na TASAF katika Shehia ya Kizimkazi Dimbani iliyopo Wilaya ya Kusini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa maelekezo ya ujenzi wa mradi wa ukumbi wa kufanyia mitihani na shughuli za kijamii unaogharamiwa na TASAF katika Shehia ya Kizimkazi Dimbani iliyopo Wilaya ya Kusini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Baadhi ya wananchi Shehia ya Kizimkazi Dimbani wakishiriki ujenzi wa mradi wa ukumbi wa kufanyia mitihani na shughuli za kijamii unaogharamiwa na TASAF katika Shehia ya Kizimkazi Dimbani iliyopo Wilaya ya Kusini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

*********************************

Na. James K. Mwanamyoto-Kizimkazi

Tarehe 29 Agosti, 2021

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imeanza ujenzi wa ukumbi utakaogharimu shilingi milioni 149 katika Shehia ya Kizimkazi Dimbani, Zanzibar ili kutatua changamoto ya kukosekana kwa darasa la kufanyia mitihani kwa wanafunzi wa eneo hilo, ambapo ukumbi huo pia utatumika kwa shughuli za kijamii kwa wananchi wa shehia hiyo iliyopo Wilaya ya Kusini Unguja.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa ukumbi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema dhamira ya ofisi yake kutumia fedha za ruzuku zinazotolewa na TASAF ni kuwasaidia wanafunzi wa eneo la Kizimkazi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihangaika kutafuta maeneo ya kufanyia mitihani.

“Mradi huu utawasaidia wanafunzi ambao wakati wa kipindi cha mitihani wamekuwa wakitafutiwa maeneo mengine ya kufanyia mitihani kutokana na kukosa darasa ya kufanyia mitihani na utawasaidia pia wakazi wa Kizimkazi kupata ukumbi wa mikutano kwani ni muda mrefu wamekabiliana na changamoto hiyo,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Ameongeza kuwa, ofisi yake kupitia TASAF imekuwa na utamaduni wa kutoa mchango kwenye jamii kwa kutoa fedha zinazotumika kuboresha huduma kwenye sekta ya elimu, afya na miundombinu kwa lengo la kuwa karibu na jamii, kushiriki utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na hatimaye wafurahie mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amesema kuwa, mradi huo wa ujenzi wa ukumbi wa kufanyia mitihani na shughuli za kijamii ulikuwa ni hitaji la wananchi wa Shehia ya Kizimkazi, hivyo TASAF ikaamua kufadhili ili kukidhi mahitaji ya wananchi hao.

“Ujenzi wa mradi huu unahusisha wananchi kufanya kazi za ajira ya muda ambapo kaya za walengwa 107 wa TASAF zinafanya kazi kwenye mradi huo,” Bw. Mwamanga amefafanua.

Bw. Mwamanga amesema, mradi huo umehusisha ushiriki wa wananchi ili waweze kutoa mchango kwenye eneo la ujenzi na kupata ujira, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kujiona ni sehemu ya mradi kwa kuchangia nguvu kazi yao.

Dhamira kuu ya ujenzi wa ukumbi huo ni kuunga mkono azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo kwa wananchi wote ikiwemo wa Shehia ya Kizimkazi ambako ndiko alikozaliwa.