Home Mchanganyiko WAKULIMA WA KIJIJI MOLE WILAYANI SIKONGE WAHIMIZWA KUPANDA MIKOROSHO ILI KUONGEZA THAMANI...

WAKULIMA WA KIJIJI MOLE WILAYANI SIKONGE WAHIMIZWA KUPANDA MIKOROSHO ILI KUONGEZA THAMANI YA ARDHI ZAO

0

Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Hussein Mchomvu akitoa elimu leo kwa wakazi wa Kijiji cha Mole jinsi kilimo cha korosho kinavyosaidia kuongeza thamani ya ardhi na kutunza mazingira.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mole Wilayani Sikonge ambao ardhi yao imerasimishwa na kupata Hati Miliki za Kimila chini ya Ofisi ya Rais, Mpango Kurasimisha Rasimali na Biashara za Wanyonge Nchini MKURABITA wakisikiliza watoa mada mbalimbali wakati wakipata elimu ya kuwajengea uwezo wa kuiongzea thamani ardhi yao ili waweze kukopesheka.

Afisa Nyuki wa Wilaya Sikonge Samwel John akitoa somo leo kwa wakazi wa Kijiji cha Mole ambao ardhi yao imerasimishwa juu ya kutumia maeneo yao kufuga kisasa nyuki ili waondokane na umaskini

Picha na Tiganya Vincent

***********************************

NA TIGANYA VINCENT

WAKULIMA wa Kijiji cha Mole wilayani Sikonge ambao maeneo yao yamepimwa na kupata hati miliki za kimila wametakiwa kutumia fursa hiyo kupanda mikorosho kwa ajili ya kuiongezea thamani ya ardhi zao.

Akitoa mada kuhusu kilimo cha korosho leo katika Kijiji Mole wilayani Sikonge Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Hussein Mchomvu alisema mikorosho ni dhahabu ya kijani ambayo inasaidia kuongeza thamani ya ardhi.

Mchomvu alisema kilimo hicho kinampa fursa mkulima kuendeleza zao hilo huku akilima mazao katikati wakati ikiwa na mwaka mmoja hadi saba ambayo yatampa kipato wakati akisubiri kuvuna korosho.

Aliongeza korosho ni mojawapo ya mazao ya kimkakati ambalo limatiliwa mkazo na wanatarajia kugawa miche kwa wananchi kwa utaratibu utakaowekwa na madiwani.

Meneja Urasimishaji Rasilimali na  Ardhi vijijini Ofisi ya Rais, Mpango Kurasimisha Rasimali na Biashara za Wanyonge Nchini MKURABITA, Anthony Temu, alisema wakati umefika kwa wananchi wa maeneo hayo kunufaika na ardhi iliyorasimishwa kwa kuiongezea thamani kwa kupanda mikorosho na miti.

Aidha Temu aliwataka wakulima kulima kilimo biashara ambacho kitawasaidia kuinuka kiuchumi toka ngazi kaya moja hadi Kijiji na Wilaya.

Afisa Nyuki wa Wilaya Sikonge Samwel John aliwataka Wakazi wa Kijiji hicho kutumia maeneo yao kuendesha ufugaji wa nyuki ambao utawasaidia kujipatia kipato na ajira.

Alisema mradi wa ufugaji wa nyuki unatoa mazao zaidi ya saba ambayo yanaweza kumuinua kikipato mfugaji na kumfanya kuwa na uhakika kipato huku akitunza na kuhifadhi mazingira.

Afisa nyuki huyo aliongeza ufugaji nyuki karibu na mashamba unaongeza mavuno kwa nyuki kusaidia kuchavusha maua.

Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Sikonge Emmanuel Mhagama alisema Benki hiyo kwa kutambua umuhimu wa kilimo katika kiunua kipato cha wananchi imeanzisha Kitengo mahususi cha kuwasaidia wakulima.

Alisema Kitengo hicho ambacho ni Kilimo Biashara kinatoa fursa kwa wakulima wenye Hati miliki za Kimila ambazo zimeongezewa thamani kupata mikopo.

Mhagama alisema kinachotakiwa ni mkulimwa ni kufungua Akaunti na kuwa na ardhi iliyongezewa thamani .

Alisema CRDB haikopeshi mtu ambaye anamiliki pori ambalo halijaongezewa thamani.