Home Mchanganyiko MWENGE MAALUM WAZINDUA JENGO LA WODI YA WAZAZI BUNGU -KIBITI NA KUONDOA...

MWENGE MAALUM WAZINDUA JENGO LA WODI YA WAZAZI BUNGU -KIBITI NA KUONDOA KERO YA UFINYU WA CHUMBA CHA KUJIFUNGULIA

0
Na Mwamvua Mwinyi,Kibiti
Wanawake wa eneo la Bungu ,Wilayani Kibiti wanatarajia kuondokana na  changamoto kubwa ya ufinyu wa chumba cha kujifungulia waliyoipata kwa zaidi ya miaka 25 iliyopita baada ya kukamilika kwa jengo la wodi ya wazazi na choo zahanati ya Bungu.
Wanawake hao kipindi hicho walitaabika kuzaa kwa mbanano na wengine kuzalia chini ,kutokana na ufinyu wa chumba na upungufu wa vitanda ambapo vilikuwa vitanda viwili .
Pamoja na hayo ,kulikuwa na kero ya maji iliyosababisha mjamzito kwenda kujifungua na maji kutoka nyumbani na vibatari kwa kukosekana nishati ya umeme.
Akizindua jengo la wodi ya wazazi na choo katika zahanati ya Bungu , kiongozi wa mbio maalum za mwenge wa uhuru ,LT.Josephine Mwambashi alisema , serikali inajitahidi kuhakikisha inaondoa matatizo ya upungufu wa majengo ya uzazi na upasuaji.
Alisema , serikali pia inapambana kutatua changamoto mbalimbali za afya ikiwemo vifaa tiba ,dawa na majengo mbalimbali.
Akitoa taarifa ya mradi mganga mfawidhi zahanati ya Bungu,Luhalala Jackson alielezea,umegharimu milioni 40 ,387,457 zikiwa ni fedha kupitia mradi wa malipo kwa ufanisi (RBF).
“Mradi huu una faida kubwa kwa wananchi wa Bungu na maeneo jirani hususan akinamama wajawazito wanaofika kituoni kwa ajili ya huduma za uzazi “
Luhalala alifafanua ,lengo ni kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga kwa kuhakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati .
Alibainisha ,wastani zahanati hiyo inahudumia wagonjwa 16,292 (OPD) ambapo wanaume ni 7,210 na wanawake 9,082 kwa mwaka ,kwa wiki wanajifungua kina mama 15 sawa na wateja 60 kwa mwezi ,ambapo kwa mwaka mzima ni wateja 400 hadi 720.
Mkazi wa Bungu ,Amina Mnjopeka alisema ,wanaishukuru serikali kwa kusogezewa huduma hiyo kwani miaka zaidi ya 20 walitaabika hasa katika tatizo la chumba kidogo cha kuzalia,maji na umeme.
Mwenge wa uhuru umepokelewa Kibiti agost 15 ukitokea Rufiji na agost 16 Jumatatu utapokelewa Wilayani Mkuranga.