Home Mchanganyiko OSHA KUTOA MAFUNZO KWA WAFANYAKAZI 6,500 SEKTA YA MAFUTA NA GESI

OSHA KUTOA MAFUNZO KWA WAFANYAKAZI 6,500 SEKTA YA MAFUTA NA GESI

0

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali kuhusu mafunzo ya huduma ya kwanza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe na washiriki wa mafunzo hayo. Gondwe alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya kuhitimisha awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yanayotarajiwa kutolewa nchi nzima.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, akizungumza na washiriki wa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa wafanyakazi wa maghala (depots) na vituo vya kuuzia mafuta vya mkoa wa Dar es Salaam. Mafunzo hayo yanatolewa na OSHA ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, akikabidhi vyeti kwa washiriki wa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa wafanyakazi wa maghala (depots) na vituo vya kuuzia mafuta vya mkoa wa Dar es Salaam. Aliyoambatana nao ni Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe (wakwanza kushoto), Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (watatu kushoto) na Mkurugenzi wa Mafunzo, Tafiti na Takwimu wa OSHA, Joshua Matiko.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, akifanyiwa vipimo vya macho na Mkaguzi wa Afya wa OSHA, Dkt. Edwin Senguo, wakati wa hafla ya kufunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya usalama na afya kwa wafanyakazi wa sekta ya mafuta na gesi Kinondoni, Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa wafanyakazi wa maghala (depots) na vituo vya kuuzia mafuta vya mkoa wa Dar es Salaam, wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, wakati wa hafla ya kufunga awamu ya kwanza ya mafunzo hayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

******************************

Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) unatarajia kutoa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi wapatao 6,500 katika sekta ya mafuta na gesi nchi nzima.

Mpango huo wa OSHA umewekwa wazi na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, alipokuwa akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo hayo katika wilaya yake ambapo amewaasa washiriki wa mafunzo kuwa mabalozi wa ujuzi walioupata katika maeneo yao ya kazi ili kuokoa maisha ya watu wanaoumia wakiwa kazini.

“Kutoa mafunzo kwa wafanyakazi 6,500 nchi nzima sio kitu kidogo hivyo OSHA wanastahili pongezi kubwa sana hasa tukizingatia kwamba malengo mahususi ya mafunzo tajwa ni kumlinda mfanyakazi na wateja wanaofika kupata huduma kwenye vituo vya mafuta. Aidha, mafunzo hayo yanalenga pia kulinda mali za wawekezaji dhidi ya majanga mbali mbali ikiwemo majanga ya moto na hivyo kuwa na uwekezaji endelevu na wenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe.

Akitoa maelezo ya awali kuhusiana na mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria Na.5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, yanatolewa kwa wawakilishi wa wafanyakazi wa maghala ya kuhifadhia mafuta pamoja na vituo vya kuuzia mafuta nchi nzima baada ya kuhitimisha ukaguzi kwenye maeneo hayo na kubaini changamoto mbali mbali za usalama na afya.

“Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi inataka kila sehemu ya kazi kuwa na wawakilishi wa wafanyakazi waliopatiwa mafunzo ya namna ya kutoa huduma ya kwanza endapo itatokea dharura kwa baadhi ya wafanyakazi kuumia ama kupata changamoto nyingine za kiafya. Hivyo, katika kuwezesha hilo, sisi tumefanya ukaguzi wa mazingira ya kazi katika depoti za mafuta pamoja na vituo vya mafuta nchi nzima na baada ya ukaguzi huo tumeanza sasa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa maeneo tuliyoyakagua,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa mwanzoni mwa juma lililopita katika Wilaya ya Kinondoni, Kassim Mtema, amesema katika mafunzo hayo washiriki wamefundishwa mada mbali kuhusiana na dhana nzima ya utoaji wa huduma ya kwanza katika maeneo ya kazi ikiwemo sheria za huduma ya kwanza, utangulizi katika huduma ya kwanza pamoja na mafunzo kwa vitendo juu ya kutoa huduma kwa wagonjwa waliopata dharura mbali mbali.

Washiriki wa mafunzo wameelezea yale waliyojifunza na umuhimu wake katika shughuli zao za kila siku hususan katika sekta ya mafuta na gesi ambayo inakuwa kwa kasi hapa nchini.

“Nimejifunza mambo mengi sana, baada ya mafunzo haya sasa nitaweza kuwahudumia wenzangu endapo itatokea changamoto yoyote ya kiusalama na afya kama vile ajali ya kuungua, kupoteza fahamu au hata kuvunjika. Kiujumla tumepata mafunzo mazuri sana, nimefunza na nimepata cheti changu hadi hapa hakika tutaweza kufanya vizuri,” ameeleza Aneth Aman ambaye alishiriki mafunzo.

Zaidi wafanyakazi 400 wa maghala na vituo vya kuuzia nishati ya mafuta wamepatiwa mafunzo ya huduma ya kwanza katika Wilaya ya Kinondoni ambapo yataendelea kutolewa katika mikoa mingine nchi nzima kwa wafanyakazi wengine zaidi ya 6,000.