Home Mchanganyiko UFAFANUZI WA TAARIFA YA UPOTOSHAJI KUHUSU UTENDAJI KAZI WA TUME YA UTUMISHI...

UFAFANUZI WA TAARIFA YA UPOTOSHAJI KUHUSU UTENDAJI KAZI WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA – LEO 13/08/2021

0

*******************************

Tume ya Utumishi wa Umma imeanzishwa chini ya Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma (Sura ya 298 marejeo ya mwaka 2019), pamoja na majukumu mengine Tume ina jukumu la kupokea na kushughulikia rufaa kutoka kwa Watumishi wa Umma na Mamlaka za Nidhamu ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa dhidi yao,  kwa mujibu wa Kifungu cha 25 (1) cha Sheria hii na Kanuni ya 60 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.

Tume ya Utumishi wa Umma inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa ya upotoshaji  kuhusu utendaji kazi wa Tume iliyotolewa kupitia mtandao wa kijamii wa “Jamii Forum” tarehe 12 Agosti 2021 kama ifuatavyo:-

  1. Kwa mujibu wa Kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019), Tume inaundwa na Mwenyekiti na Wajumbe 6 ambao huteuliwa na Rais ambao pamoja na majukumu mengine wana jukumu la kisheria la kutolea uamuzi rufaa na malalamiko yanayowasilishwa mbele ya Tume. Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 14(1) na (2) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019),   Tume ina Katibu ambaye ndiye Mtendaji Mkuu. Katibu na Wasaidizi wake (Sekretarieti) ndio watendaji wa kazi za kila siku katika Tume ya Utumishi wa Umma ambao wameteuliwa baada ya kukidhi sifa na vigezo katika nafasi walizo nazo.
  2. Pamoja na Sheria zilizopo, Tume inashughulikia rufaa kwa mujibu wa Mwongozo Kuhusu Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2009 ambapo rufaa hupokelewa, husajiliwa, huchambuliwa na kupitiwa na Kikao cha Menejimenti na hatimaye kuwasilishwa mbele ya Tume kwa uamuzi. Hatua ya mwisho ni Mrufani na Mrufaniwa kujulishwa kwa barua juu ya uamuzi unaotolewa na Tume. Utaratibu huu umewekwa ili kuimarisha utendaji kazi, kudhibiti upendeleo, rushwa na kuimarisha utoaji wa haki. Aidha, elimu kuhusiana na utaratibu huu imekuwa ikitolewa kwa wadau kupitia majukwaa mbalimbali.
  3. Tume katika kushughulikia rufaa na malalamiko haitoi uamuzi kwa shinikizo au ushawishi wa Mwajiri au Mamlaka ya Nidhamu yoyote ili kuwakandamiza watumishi wasipate haki zao. Tafsiri kuwa Tume ni chombo cha kulinda maslahi ya Waajiri na Serikali. Tume inapenda kuufahamisha umma kuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo.

 

  1. Rufaa na malalamiko yanayopokelewa Tume yenye vielelezo vilivyokamilika ndio yanayoshughulikiwa na kutolewa uamuzi kwa kadri yalivyopokelewa (First in, First Out).

 

  1. Tume ya Utumishi wa Umma, inaomba umma kuupuuza upotoshwaji huu uliotolewa kupitia mtandao wa kijamii wa “Jamii Forum” na inatoa wito kwa umma na wadau wote kuwasiliana na Tume kwa ufafanuzi, maoni au suala lolote kuhusu Tume kupitia simu namba 0738166703, 0733 005 974 na barua pepe, [email protected].

Imetolewa na:

 

John C. Mbisso

KAIMU KATIBU

TUME YA UTUMISHI WA UMMA

DAR ES SALAAM