Home Mchanganyiko KATIBU MTENDAJI SADC AAGA,AITAKA SADC KUIMARISHA UWEZO WA NDANI KUTENGENEZA DAWA NA...

KATIBU MTENDAJI SADC AAGA,AITAKA SADC KUIMARISHA UWEZO WA NDANI KUTENGENEZA DAWA NA CHANJO ZA MAJANGA NA MAGONJWA YA MILIPUKO

0

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata (Mb) Mulamula akiwa katika Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC. Kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) na kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardius Kilangi. Kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa SADC kinafanyika hii leo Agosti 13,2021 Lilongwe – Malawi.  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) (kushoto) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardius Kilangi (kulia). Viongozi hao wako Lilongwe – Malawi kuhudhuria Mkutano 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaotarajiwa kufanyika 17 -18 Agosti,2021

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax akiteta jambo na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb). Kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) kushoto kwa Balozi Mulamula ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardius Kilangi akifuatiwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda Balozi Agnes Kayola.

 

*****************************

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC imetakiwa kuimarisha uwezo wa ndani wa kutengeneza chanjo na dawa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa dawa na chanjo panapotokea majanga na magonjwa ya milipuko inayosababisha vifo vingi katika Bara la Afrika.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC Dkt. Stergomena Tax ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya utendaji ya Jumuiya hiyo katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC na kuongeza kuwa janga la UVIKO -19 limekuwa na changamito kubwa husasani katika upatikanaji wa chanjo kwa wananchi wote wa Jumuiya hiyo.

Dkt. Tax ambaye ameitumia fursa hiyo kuwaaga Mawaziri wa SADC kutokana na kumaliza muda wake amezisihi nchi za Afrika kuweka nguvu za pamoja katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 na kuziomba Nchi,Taasisi na Jumuiya za Kimataifa kuridhia nchi masikini ziwezo kutumia teknolojia zao katika kuzalisha dawa na chanjo ili huduma hiyo ipatikane kwa wananchi wote.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ambaye ameongozana na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Prof. Adelardus Kilangi amezitaja baadhi ya ajenda zitakazojadiliwa katika Mkutano huo kuwa ni pamoja na kumchagua mwenyekiti mpya wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba kwa upande wake amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano katika kufuata sharia na taratibu za Jumuiya mbalimbali ambazo Tanzania ni mwanachama ikiwa ni pamoja na ulipaji wa ada kwa wakati.

Mkutano huu wa siku mbili wa Baraza la Mawaziri wa SADC ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 17 na 18,Agosti 2021 Lilongwe nchini Malawi na Tanzania itawakilishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo pamoja na mambo mengine utaidhinisha nyaraka mbalimbali za kisheria ikiwemo itifaki ya takwimu.