Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Uzini Khamis Hamza Chilo (kulia)akishirikiana na Mwakilishi Haji Shaaban Waziri(kati)wakipokea msaada wa Taulo za kike kutoka kwa Bwana Dominicus M. Ulikaye kutoka kampuni ya Human Cherish Pads.
Mbunge wa Jimbo la Uzini Khamis Hamza Chilo na Mwakilishi Haji Shaaban Waziri wakifurahia kwa pamoja na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Mwera mara baada ya kupatiwa msaada waTaula za kike na elimu kuhusu Hedhi Salama.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Uzini akigawa Taulo za kike kwa Wanafunzi wa Skuli ya Msingi na Sekondari ya Kidimni.
**************************************
Bahati Habibu Maelezo Zanzibar 12/8/2021.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Uzini Khamis Hamza Chilo, amewataka wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Kidatu cha Nne kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu vizuri .
Ameyasema hayo wakati alipokutana na wanafunzi wa kike wanaokaa kambi katika ziara yakuzitembelea Skuli mbalimbali za Sekondari na kuwapatia Taula za kike zilizotolewa msaada na kampuni ya Human Cherish kutoka China yenye Tawi lake Tanzania ambazo zitawasaidia kwa usalama wa afya zao.
Amesema mara nyingi watoto wa Kike hupata usumbufu na wakati mwengine kushindwa kuhudhuria vipindi vya masomo kutokana na msongo wa mawazo au kujiskia vibaya kutokana na kukosekana njia bora ya kujihifadhi.
Aidha amewataka Walimu wakike kuwa karibu na wanafunzi hao ili kuwasaidia katika kutatua Changamoto wanazokutana nazo katika mazingira ya utafutaji wa elimu jambo ambalo litawawezesha kufikia ndoto zao.
“Watoto wetu hawa huwa wanakutwa na mambo mengi ikiwemo kufanyiwa udhalilishaji na watu wao wa karibu ila huwa wanakosa msaada wa haraka kutokana na kukosa watu wa kuwaeleza majumbani na hata shuleni matokeo yake ni kushindwa kuendelea na masomo kwa kufeli au kupata Mimba wakiwa Shuleni “ alisema Waziri Chilo.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Haji Shaaban Waziri, amesema msaada huo wa Taulo za kike umekuja wakati muwafaka kutokana na wanafunzi wa Kidatu cha Nne kuwepo Mashuleni wakisoma kwa pamoja ili kujiandaa na Mtihani wa Taifa.
Amesema wazee wengi wa watoto hao hawana uwezo wa kuwanunulia kila Mwezi Taulo zilizosalama kwa Afya zao na badala yake hutumia njia ya asili ya kujihifadhi ambayo haipo salama na inauwezekano mkubwa wa kuleta magonjwa ya UTI na Fangas hatimae kusababisha maambukizi katika njia ya uzazi au Ugumba.
Aidha amewataka wanafunzi hao wa kike kuitumia elimu waliyopatiwa kuhusu kujihifadhi ili waweze kujilinda na kuwalinda wengine kwa kuwafikishia elimu waliopatiwa.
Nae Mwakilishi wa HC Tanzania Ummul-Kulthum Asit Khan amesema msaada huo una lengo la kuwaelimisha watoto wa kike kuhusu hedhi salama sambamba na kuwafahamisha namna ya kujistiri wakati wa hedhi ili waweze kuendelea na masomo katika hali hiyo.
Aidha amewasititiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujiepusha na vishawishi mbalimbali vitakavyosababisha kutokufikia malengo yao.
Nao Wanafunzi waliopatiwa msaada huo wa taula za kike wamewashukuru viongozi wa Jimbo hilo na kuahidi kuitumia elimu waliopewa ili kuepukana na changamoto wanazokumbana nazo katika kipindi cha masomo.
Aidha wamewaomba Viongozi hao kuendelea kuwapatia misaada mengine ikiwemo chakula kwa muda wote wanaokaa kambi ili kupata wakati mzuri wa kudurusu masomo yao.