Home Mchanganyiko KAMATI YA ELIMU,AFYA NA MAJI WILAYANI BUSEGA YATAKA UBORESHWAJI WA MIUNDOMBINU MASHULENI

KAMATI YA ELIMU,AFYA NA MAJI WILAYANI BUSEGA YATAKA UBORESHWAJI WA MIUNDOMBINU MASHULENI

0

Na Mariane Mariane Mgombere, Busega-Simiyu

Kamati ya Elimu, Afya na Maji ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega imetaka kuboreshwa kwa miundombinu katika mashule ili kutengeneza mazingira rafiki zaidi kwa Walimu na Wanafunzi. Kamati hiyo ambayo imefanya ziara ya siku moja katika Shule za Msingi za Ilumya na Mwabuduli  kwa lengo la kukagua miundombinu siku ya tarehe 03 Agosti 2021.

Akiongoza ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vumi Magoti amesema kuna uhusiano mkubwa wa mazingira ya Shule na elimu bora kwa Wanafunzi. Baadhi ya changamoto zilizogunduliwa na Kamati hiyo ni pamoja na kutokuwepo kwa nishati ya umeme katika makazi ya Walimu, uchache wa madarasa, huduma isiyoridhisha ya vyoo na Uhaba wa Nyumba za Watumishi.

Afisa Mipango na Ufuatilia Wilaya ya Busega Bw. Juma Rahisi amesema ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Shule unafanyika kwa kuzingatia mahitaji ya Shule husika hivyo miundombinu ya Shule hizo itaboreshwa kama ilivyo kwa Shule nyinginezo. Aidha, Bw. Rahisi amewataka viongozi wa Shule kutoa ripoti za mazingira ya Shule mara kwa mara ili kufanyiwa kazi. “Kama kuna mtu ana changamoto yoyote tuwe tunaonana ili kuelezana changamoto”, aliongeza Bw. Rahisi.

Kwa upande wao, Walimu Wakuu wa Shule zote mbili wameshukuru kwa kutembelewa na Kamati hiyo, pia wameomba changamoto ndogondogo zilizopo katika Shule hizo na nyinginezo kufanyiwa kazi ili kuwa na mazingira rafiki katika majukumu yao ya kila siku.

Kamati imefanya ziara katika Shule hizo mbili zilizopo Kata ya Kiloleli ili kuona changamoto zilizopo na kuzifanyiwa kazi. Katika ziara hiyo pamoja na Waheshimiwa madiwani pia Watendaji waliweza kuhudhuria.