Home Mchanganyiko SGA SECURITY YAPONGEZWA KWA KUJALI WAFANYAKAZI

SGA SECURITY YAPONGEZWA KWA KUJALI WAFANYAKAZI

0

Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Bw. Ramadhan Kingai (kulia) akitoa zawadi kwa mmoja wa wastaafu wa kampuni ya SGA Security wakati wa hafla maalumu ya kuwaaga wastaafu 40 wa kampuni hiyo huku Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Eric Sambu (katikati) akishuhudia.

********************

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kampuni ya SGA Security imepongezwa kwa rekodi yake maalumu ya kuhakikisha wafanyakazi wake wanadumu kwa muda mrefu hadi umri wa kustaafu tofauti na makampuni mengine.

Akizungumza katika hafla maalumu ya kuwaaga wastaafu 40 wa SGA, Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Bw. Ramadhan Kingai ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kampuni ya SGA security inastahili kuigwa na makampuni mengine.

Bw Kingai aliwapongeza wastaafu hao kwa kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kuongeza kuwa walinzi wengi hushawishika kuingia katika ujambazi kwa sababu ya changamoto wanazozipata kazini.

“Nawaomba mkawe mabalozi wazuri wa amani katika jamii. SGA imedhihirisha ya kuwa inawajali wafanyakazi wake wanaobaki na wanaoondoka kwani mikataba ya kazi haioneshi popote kuwa mfanyakazi atapewa zawadi wakati wa kustaafu lakini SGA imeingia gharama hiyo, ni jambo la kupongezwa,” alisema.

Alitoa pongezi kwa uongozi wa kampuni hiyo kwa kuwa mfano pia katika kuhakikisha makato ya wafanyakazi yanawasilishwa kwa wakati na kuwahakikishia wafanyakazi kuhusu pensheni zao, tofauti na makampuni mengine ambako kuna malalamiko mengi.

Kamanda huyo pia alishukuru uongozi wa kampuni hiyo kwa ushiriano na Jeshi la Polisi na kwamba kampuni hiyo imeendelea kutoa huduma za viwango vya juu na kuendelea kulisaidia Jeshi la Polisi katika kuhakikisha kuna utulivu na wananchi wanafuata sheria.

“Makampuni binafsi ya ulinzi ni sehemu ya Polisi Jamii. Kuna amani na utulivu nchini kwa sababu ya ushirikiano tunaopata kwenu,” alisema na kuongeza kuwa SGA ndio kampuni pekee ya ulinzi ambayo huomba msaada wa Jeshi la Polisi katika kutoa mafunzo kwa walinzi wake wapya jambo ambalo hufanya walinzi hao kuwa bora zaidi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Security, Bw. Eric Sambu alisema waanzilishi wa kampuni hiyo walihimiza nidhamu ya hali ya juu kwa uongozi kuhakikisha wanayapa kipaumbele masilahi ya wafanyakazi. Hii alisema ndio siri ya mafanikio ya kampuni hiyo.

SGA ndio kampuni kongwe binafsi ya ulinzi nchini iliyoanzishwa mwaka 1984 huku ikijulikana kama Group 4 Security. Kwa sasa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 5000 nchi nzima.

SGA ndio kampuni pekee ya ulinzi yenye cheti cha ISO 18788 – Security Operations Management System.

SGA Security inatoa huduma mbalimbali ikiwemo za ulinzi, alarm, huduma za fedha, ulinzi wa kielektroniki, huduma ya kusafirisha mizigona huduma nyinginezo.

Mwaka huu kampuni hiyo ilipokea tuzo baada ya kutangazwa mshindi wa jumla kama kampuni yenye rasilimali za kutosha na ya kuaminika (Most Equipped and Reliable Security Company of the Year, 2020) katika tuzo za chaguo la wateja (Consumer Choice Award).